Amina siri ya mafanikio nyuma ya Ajibu

Muktasari:

Ajibu amerudi nyumbani pale Msimbazi kwani, alikulia hapo kabla ya kwenda Jangwani miaka miwili iliyopita na kuifungia mabao saba pamoja na pasi za mwisho 17.

IBRAHIM Ajibu ni jina ambalo limeteka vyombo vya habari kinoma baada ya kumaliza mkataba wake na Yanga huku akihusishwa na kutua TP Mazembe ya DR Congo na Simba.
Lakini Julai 3, uongozi wa Simba ulikata mzizi wa fitna kwa kumtambulisha kama mchezaji mpya kwa mkataba wa miaka mitatu akitokea Yanga ambako alipewa jukumu la kuwa kiongozi wa wenzake uwanjani.
Ajibu amerudi nyumbani pale Msimbazi kwani, alikulia hapo kabla ya kwenda Jangwani miaka miwili iliyopita na kuifungia mabao saba pamoja na pasi za mwisho 17.
Achana na ishu za nyota huyo ndani ya uwanja huko nje ni hatari na hapa Mwanaspoti linakuletea maisha yake nje ya soka unaambiwa ni mzazi bora kwa familia yake.
Mwanaspoti limefanya mazungumzo na mke wa kiungo huyo mshambuliaji Amina Ajibu, ambaye amefunguka kuwa hajuti kukutana naye kabisa.

MUME BORA
Wadau wa soka wanamfahamu Ajibu kama mtu asiyependa maneno mengi na hutoa kipaumbele zaidi kwa vitendo uwanjani, basi unaambiwa akiwa nyumbani mambo yake kwa mkewe ni tofauti na anavyochukuliwa.
“Mume wangu pamoja na kuonyesha ufundi uwanjani kwa ari ya juu, basi uchovu wake unaishia huko huko, akiwa hapa majukumu yake ya kifamilia anatimiza kwa wakati bila ya visingizio,” anasema.

BABA BORA
Migomba ni baba wa mtoto mmoja wa kike inayeitwa Ahlam na unaambiwa mfanyie vyote hata ukimtukana atachukulia poa, lakini ukileta ishu za kizushi kwa mwanaye huyo, basi patachimbika buana.
Unaambiwa furaha ya Ajibu ni kumuona binti yake huyo kila wakati na ikipita saa mbili hajamuona, basi hupiga simu hata mara sita kikubwa ni kuulizia maendeleo ya mwanaye.
“Kuhusiana na Ahlam sijui nikwambie nini unielewe, mapenzi kwa mwanaye ni makubwa sana. Hawezi kulala kama mwanaye yupo macho na anapenda kufua mwenyewe nguo za mwanaye hata kama kachoka,” anasema.

KUPIKA MMH
Ule udambwi udambwi wake uwanjani namna ya kupiga pasi za mwisho na faulo matata za mwana ukome, basi hayo mambo yanaishia huko uwanjani. Huko nyumbani unaambiwa Ajibu hajui hata sufuria linatengwa vipi jikoni.
“Tangu nimeanza uhusiano na Ajibu sijawahi kumuona wala kumsikia akizungumzia ishu za kuingia jikoni. Hata hafahamu sufuria zinakaa sehemu gani jikoni,” anasema.

HAPOTEZI ATA
SEKUNDE KWENYE KULA
Pamoja na kushindwa kuingia jikoni kupika, lakini kwenye suala la maakuli jamaa huwa hanaga muda wa kupoteza kabisa. Ratiba yake ni kugonga msosi mara tatu kwa siku na hajawahi kupiga deshi.

HAPENDI DHARAU
Basi ukitaka kugombana na Ajibu muonyeshe dharau ni kitu ambacho kinamkwaza na huwa anagombana na wengi wanaomfanyia hivyo.
“Mume wangu hapendi vitu vyote vibaya, lakini kama mnataka kununiana, basi wewe mdharau tu na hapo utaona moto wake,” anasema.