Kocha Klopp awatia presha mabosi wake Liverpool

Muktasari:

Wamiliki wa klabu ya Liverpool, Fenway Sports Group wanataka Klopp asaini mkataba mpya wa miezi sita kwenye kikosi hicho wenye thamani ya Pauni 60 milioni, ili kumkinga asije kubebwa na klabu nyingine vigogo huko Ulaya.

LIVERPOOL, ENGLAND. LIVERPOOL wanahofu kwamba uchovu unaweza kumfanya kocha wao Jurgen Klopp akafanya uamuzi wa kutosaini dili la mkataba mrefu wa kuendelea kuinoa klabu hiyo yenye maskani yake huko Anfield.
Kocha huyo Mjerumani kwa sasa analipwa mshahara wa Pauni 7 milioni kwa mwaka, pesa ambayo imedaiwa kwamba itaongezeka kwa Pauni 3 milioni kama atasaini dili jipya baada ya mabosi wa timu hiyo kufurahishwa na huduma yake kufuatia taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya alilowapa msimu uliopita.
Wamiliki wa klabu ya Liverpool, Fenway Sports Group wanataka Klopp asaini mkataba mpya wa miezi sita kwenye kikosi hicho wenye thamani ya Pauni 60 milioni, ili kumkinga asije kubebwa na klabu nyingine vigogo huko Ulaya.
Lakini, Klopp anadai kwamba afya ni kitu kikubwa zaidi kwake kuliko pesa, ndiyo maana anachukua muda kufanya uamuzi kuhusu kusaini dili refu kwenye klabu hiyo ya Liverpool.
Hakuna maana kwamba Klopp anafikia kuipiga kibuti Liverpool kabla ya mkataba wake wa sasa kufika mwisho, lakini aliondoka Borussia Dortmund baada ya kukaa kwa muda kwenye timu hiyo, kitu ambacho alikifanya hivyo pia alipokuwa na Mainz. Klopp alitua Liverpool mwaka 2015 alipochukua mikoba ya Brendan Rodgers.
Kumekuwa na taarifa kwamba klabu za Juventus na Real Madrid zilikuwa na mpango wa kumnansa kocha huyo kabla ya kuwachukua Maurizio Sarri na Zinedine Zidane. Na sasa kitendo cha kuchukua muda mrefu kabla ya kuamua kusaini dili jipya linawapa wasiwasi mabosi wake huko Anfield.