Mabadiliko Uefa kuja na mfumo kuziokoa Manchester United, Arsena

Muktasari:

Mpango huo mpya ukifanikiwa, basi kwa timu za Ligi Kuu England kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu unaokuja haitahitaji kumaliza ndani ya Top Four kwenye ligi ya ndani, bali kumaliza nafasi za juu kwenye michuano ya msimu uliopita kwenye ligi ya Ulaya.

NYON,USWISI. Mambo yanakwenda haraka. Miaka michache baadaye hutohitaji uwepo kwenye Top Four kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu unaokuja. Mambo yatakuwa yamejipanga yenyewe tu.
Mambo yako hivi. Shirikisho la soka la Ulaya, Uefa linafikiria kufanya mabadiliko ya mfumo wa kufuzu Ligi ya Mabingwa Mabingwa Ulaya jambo ambalo linaweza kuzisaidia sana klabu za Ligi Kuu England.
Mpango huo mpya ukifanikiwa, basi kwa timu za Ligi Kuu England kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu unaokuja haitahitaji kumaliza ndani ya Top Four kwenye ligi ya ndani, bali kumaliza nafasi za juu kwenye michuano ya msimu uliopita kwenye ligi ya Ulaya.
Bosi wa Uefa, Aleksander Ceferin alisema wapo kwenye majadiliano kwa sasa ya kuzilinda timu zinazofika hatua za juu kabisa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya ili kupata nafasi ya kucheza kwenye michuano hiyo msimu unaofuatia.
Ipo hivi, kama klabu inafika nusu fainali kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu, basi inapaswa kupewa nafasi ya kucheza michuano hiyo kwa msimu unaofuatia bila ya kujali wameshika nafasi ya ngapi kwenye ligi yao ya ndani.
Mpango huo utazipa nafasi pia timu zilizofika hatua ya robo fainali kucheza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu, kufuzu kwenye msimu unaofuatia, kitu ambacho kinaweza kuifanya Ligi Kuu England kuwa na timu zaidi ya nne kwenye msimu mmoja wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mfumo wa sasa unaotumika kwa timu za Ligi Kuu England kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya ni ule wa kuhakikisha wanashika nafasi nne za juu jambo ambalo limekuwa na ushindani mkali zaidi siku za karibuni.
Kwenye Ligi Kuu England kuna vigogo kama Manchester United, Manchester City, Liverpool, Arsenal, Chelsea na Tottenham Hotspur ambao wanafanya Top Four inayotoa tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kuwa na upinzani mkali.
Utaratibu huo mpya, unaweza kupunguza vita ya Top Four, lakini ukienda kuongeza upinzani zaidi Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa sababu timu inafahamu kumaliza nafasi za juu huko kuanzia robo fainali kutawapa tiketi ya kucheza tena michuano hiyo kwa msimu unaofuatia.
Kwa mfano, Man United ilifika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita, lakini msimu ujao haitakuwapo kwenye michuano hiyo kwa sababu wamemaliza nafasi ya sita kwenye ligi yao ya ndani.
Mabadiliko hayo yanayokwenda kufanywa yamelenga zaidi kuzifanya timu kulinda wachezaji wao muhimu pia kwa sababu wanafahamu wazi kama watakuwa wameishia kwenye hatua ya kuanzia robo fainali kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya watakuwa na nafasi ya kucheza tena michuano hiyo msimu unaofuatia bila ya kujali nafasi zao walizomaliza kwenye ligi za ndani. Ceferin alisema majadiliano zaidi ya jambo hilo yamepangwa kufanya Septemba 11 na kusema:  “Tungependa kuzilinda timu kama Ajax mwaka huu, au Monaco na Leicester City ambazo ziliwahi kufika hatua ya robo fainali huko nyuma.
“Ajax wamefika nusu fainali mwaka huu, lakini sasa wanauza tu wachezaji wao kwa sababu hawana uhakika kama watafuzu tena kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka mwingine. Huu nadhani ni mfumo ambao utaziokoa baadhi ya klabu katika misingi hiyo. Mjadala mwingine unaopangwa kujadiliwa na Uefa ni kuhusu mfumo mpya unaopendekezwa kutumika kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya timu sasa ziongezeke kufikia 40 au 48 na zitapangwa kwenye makundi manne yatakayokuwa na timu nane. Awali kulikuwa kuwa na makundi manane yenye timu nne kila moja.