Kisa Bafana Bafana: Rais FA Misri ajiuzulu, kocha atimuliwa

Muktasari:

Uamuzi huo mgumu umekuja saa chache baada ya wenyeji wa Fainali za Kombe la Mataifa Afrika,Misri kutolewa kwa mshtuko na Afrika Kusini katika mchezo wa hatua ya mtoano ya 16 bora.

Dar es Salaam. Rais wa Chama cha Soka Misri, Hany Abou-Rida amemtimua kocha mkuu wa timu ya taifa hilo Janvier Aguirre huku mwenyewe akitangaza kujiuzulu nafasi yake.

Uamuzi huo wa Abou-Rida unakuja yakiwa yamepita saa chache tangu Misri wenyeji wa Fainali za Afcon kutolewa kwa mshtuko na Afrika Kusini 'Bafana Bafana' katika mchezo wa hatua ya 16 bora wakipokea kipigo cha bao 1-0.

Katika taarifa yake Abou -Rida amesema sababu kubwa ya kumfuta kazi Aguirre raia wa Mexico ni kufuatia matokeo hayo ambayo hawakuyatarajia.

Hata hivyo mapema Aguirre kabla ya kuanza kwa fainali hizo aliwahi kusema kama hataweza kuipa mafanikio ya ubingwa Misri ataachia ngazi katika nafasi hiyo.

Aguirre amekubali kubeba msalaba huo kwa kuwa muwajibikaji mkuu ni yeye huku akiwapongeza wachezaji wake akisema kutotumia nafasi kwenye mchezo huo kumewaghalimu.

Abou-Rida pia ameamua kuachia ngazi akisema matokeo hayo hayampi heshima ya kuongoza soka la Misri huku akiwataka wajumbe wake pia kuchukua uamuzi huo kulipa heshima soka la nchi yao.

Tayari wajumbe wanne wa chama hicho Hazem Imam, Magdy Abdel Ghani, Saif Zaher na Ahmed Megahed wamechukua uamuzi huo wa kujiuzulu mara moja kutokana na matokeo hayo.

Licha ya kujiuzulu Abou-Rida ataendelea kuongoza kamati ya kusimamia fainali hizo mpaka Julai 19 atakapoanza rasmi kutumikia maamuzi yake ya kujiuzulu.

Mashabiki wa soka nchini Misri ingawa wameumizwa na matokeo hayo lakini wengi wameonyesha kutoshangazwa na matokeo hayo kutokana na tangu kuanza kwa fainali hizo huku timu yao ikishinda mechi tatu za awali hawakuwa wanaridhika na kiwango cha timu yao.

Mashabiki hao wamekuwa wakimpigia kelele staa wao Mohamed Salah wakitaka ajitume zaidi na kuwaamsha wenzake wanapokuwa uwanjani.

uamuzi huo yanakuwa tofauti kutokana na mashabiki wa Bafana Bafana ambao nao hawakuwa na imani na timu yao kama inaweza kufika mbali hata kupata ushindi huo mbele ya Misri.

Kiungo wa Bafana Bafana, Bongani Zungu amesema baada ya mashabiki wao kutowapa nafasi kocha wao Stuart Baxter aliwataka kupambana kwa ajili ya mashabiki hao, familia zao na kwa timu yao hatua ambayo imewapa ushindi huo mkubwa.