Mkenya kuchezesha Afcon leo, Harambee Stars iko tayari kuivaa Senegal

Muktasari:

Waweru ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta cha Kilimo na Teknolojia, atasaidiana na Mkenya mwenzake, Gilbert Cheruiyot, na Mlesotho Souru Phatsoane.

Cairo, Misri. Mkenya Peter Waweru ataweka historia ya kuwa Mwamuzi wa kwanza kutoka Kenya, kuchezesha mechi katika fainali zinazoendelea za mataifa ya Afrika (Afcon), atakapopuliza kipyenga katika mchezo mkali wa Kundi D, kati ya Namibia na Ivory Coast.

Ukiwa ni mchezo wake wa kwanza tangu ateuliwe na shirikisho la soka la Afrika, miongoni wa waamuzi wanaocheza makala haya ya 32, Waweru, ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta cha Kilimo na Teknolojia, atasaidiana na Mkenya mwenzake, Gilbert Cheruiyot, na Mlesotho Souru Phatsoane.

Wakati Waweru akiingia dimbani kwa mara ya kwanza, mwamuzi msaidizi Gilbert Cheruiyot, yeye atakuwa anachezesha mechi yake ya pili, kwani Juni 29, alishika bendera wakati Ghana na Cameroon iliyomalizika kwa sare tasa.

Mbali na mechi hiyo, ambayo ni muhimu kwa Ivory Coast maarufu kama Tembo, ambao ni mabingwa wa mwaka 2015, itakayopigwa katika uwanja wa Jeshi, kutakuwa na mechi zingine tatu kali ikiwemo mechi za Kundi C, itakayoshuhudia Kenya na Tanzania, zikishuka dimbani, kuanzia saa nne usiku, kuvaana na Senegal na Algeria mtawalia.

Harambee Stars iko tayari

Wakati huo huo, Morali imeongezeka katika kikosi cha timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, kuelekea mchezo wao wa mwisho Kundi C, dhidi ya Simba wa milima ya Teranga, utakaopigwa leo kuanzia saa nne usiku, kufuatia kurejea kwa mabeki wawili waliokuwa majeruhi.

Kenya iko katika nafasi ya tatu kwenye msimamo, ikiwa na pointi zake tatu, sawa na Senegal, inayoshika nafasi ya pili, wakizidiana kwa tofauti ya mabao tu, na hivyo inahitaji kushinda au kulazimisha sare katika mechi hiyo ya kukata na shoka itakayopigwa kwenye dimba la Jeshi la Cairo.

Kwa mujibu wa Kocha mkuu wa Stars, mfaransa Sebastien Migne, beki kisiki wa kati Joash 'Berlin Wall' Onyango yuko fiti kucheza mechi ya leo, baada ya kukosa mechi mbili za awali dhidi ya Alegeria na Tanzania, baada ya kuumia mazoezini.

Mbali na Onyango ambaye kurejea kwake kumepokelewa kwa shangwe na wenzake pamoja na mashabiki wa soka nchini, nyota mwengine aliyerejea kikosini ni beki wa kulia, Philemon Otieno, aliyekosa mechi ya Tanzania, huku beki ya kati nayo ikikosa ubabe na uongozi wa 'Berlin Wall'.