Sikia Neymar alichosema huko Barcelona

Muktasari:

Hali ya mambo ilivyo, Neymar ni kama vile ameshamalizana na PSG kwamba anaweza asionekane tena uwanjani akiichezea timu hiyo ikiwa ni miaka miwili tu imepita tangu ulipofanyika uhamisho wake wa pesa nyingi Pauni 198 milioni na kuvunja rekodi ya dunia.

BARCELONA, HISPANIA. SUPASTAA, Neymar amewaambia marafiki zake wa karibu huko Camp Nou akiwambia: "Ondoeni wasiwasi, nakuja."
Ishu ya Neymar kurudi Barcelona imekuwa siriazi kwa sasa huku ripoti nyingine zikidai kwamba huenda Mbrazili mwenzake, Philippe Coutinho akahusika kwenye uhamisho huo akiondoka Nou Camp kwenda kujiunga na Paris Saint-Germain atakakokuwa anatoka fowadi huyo.
Hali ya mambo ilivyo, Neymar ni kama vile ameshamalizana na PSG kwamba anaweza asionekane tena uwanjani akiichezea timu hiyo ikiwa ni miaka miwili tu imepita tangu ulipofanyika uhamisho wake wa pesa nyingi Pauni 198 milioni na kuvunja rekodi ya dunia.
Lakini, rekodi hiyo inaweza kuvunjwa kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi baada ya wababe wawili wa La Liga, Barcelona na wapinzani wao Real Madrid wakichuana vikali kuwania huduma ya staa huyo.
Suala la kurudi Barca linaonekana kama ndilo lenye nafasi zake baada ya Neymar kuwaambia mastaa wenzake wa zamani wa timu hiyo ambao wamekuwa marafiki na kutengeneza grupu la WhatsApp, kwamba wasiwe na hofu, yeye anarudi kwenye timu hiyo.
Neymar amefunga mabao 51 katika mechi 58 alizochezea PSG, lakini amejikuta amechoka kuitumikia timu hiyo kutokana na kukosekana ushindani kwenye Ligue 1. Ripoti zinadai kwamba Neymar amemwambia mwenyekiti wa PSG, Nasser Al-Khelaifi kwamba hataichezea timu hiyo tena, anataka kurudi nyumbani, ambako ni Barcelona.
Kwa mujibu wa The Times, Barca wamejiandaa kulipa Pauni 90 milioni pamoja na mchezaji mmoja au wawili kwa ajili ya kumnasa Neymar arudi kwenye kikosi chao huko Nou Camp. Hata hivyo, Neymar hatashusha mshahara wake atakapotua huko Nou Camp, hivyo mabosi wa Barca watarekebisha mambo yao kuhakikisha Lionel Messi anaendelea kubaki kuwa mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa zaidi kwenye kikosi hicho.