Mbona iko hivi: Ukweli ni kuwa hawajali kuhusu Tanzania

Muktasari:

Kama kweli tunataka kufanya vizuri huko mbele, ni muhimu kama nchi tukajiwekea utaratibu wa kutengeneza makocha wetu.

KOCHA Mkuu wa Senegal (Simba wa Teranga), Aliou Cisse na Kocha Mkuu wa Algeria (Mbweha wa Jangwani), Djamel Belmadi, ni marafiki wa tangu utotoni. Wamekulia pamoja katika viunga vya Jiji la Paris, Ufaransa. Wanajuana vema kiuchezaji na hata kiufundi.
Ingawa wamekulia Ulaya, hawa ni watoto wa masikini na waliishi katika maeneo ambayo ilibidi mtu awe na ngozi ngumu kumudu maisha. Ndiyo sababu, wote wawili walijulikana kama wachezaji ‘chuma’ nyakati zao za uchezaji.
Makocha wa Tanzania (Taifa Stars), Emmanuel Amunike na mwenzake wa Kenya, Sebastien Migne, hawajuani. Mmoja ni Mfaransa aliyekulia kwao na mwingine ni Mnigeria, ambaye ilibidi akulie kwao kidogo kabla ya kuondoka kwenda kutafuta maisha ughaibuni na kucheza kwa kiwango cha juu.
Senegal inakwenda Misri kushiriki mashindano ya AFCON ikiwa timu inayoshika namba moja kwa kiwango cha soka cha barani Afrika. Na ingawa haipewi nafasi ya kutwaa ubingwa, Algeria imewahi kushika namba moja miaka michache tu iliyopita na si timu ambayo inabezwa kwenye mashindano haya.
Hakuna anayejali kuhusu Tanzania au Kenya. Wachambuzi wengi wa soka nje ya nchi zetu wanaamini Tanzania, Kenya, Burundi, Madagascar na nchi nyingine zilizofuzu zilifanikiwa kwa sababu tu ya uamuzi wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuongeza idadi ya timu washiriki kutoka 16 mpaka 24.
Kama Michael Jackson alivyopata kuimba kupitia wimbo wake maarufu wa “They Don’t Care About Us”, kusema ukweli wengi hawajali sana kuhusu nini hasa Taifa Stars itafanya katika mashindano haya.
Si vigumu sana kung’amua kwanini Tanzania wala Kenya si mojawapo ya timu zinazotarajiwa kung’ara. Unaweza kufahamu kwa kuwafahamu washindani wa timu hizo, wahusika wa benchi la ufundi na historia za timu husika.
Benchi la Ufundi
Nimeanza makala yangu kwa kuwatazama Cisse na Belmadi. Lakini ningeweza pia kutumia mifano ya watu kama Herve Renald wa Morocco, Javier Aguirre wa Misri na makocha wengine wa kiwango hicho.
Cisse ni mzalendo wa Senegal. Lakini, elimu yake yote ya soka ameipata  Ufaransa kuanzia angalia mdogo. Anazungumza Kifaransa na anasikiliza mafunzo na kusoma majarida kwa kupitia lugha hiyo ya kigeni pasipo shida.
Lakini pia ni mchezaji wa kiwango cha juu cha soka na wachezaji anaowafundisha wamewahi kumuona akicheza, wanamheshimu na kuamini katika mbinu zake. Bahati nzuri, naye anawafahamu wachezaji wao na tabia za kikwao. Kwa kifupi, anaenda nao sambamba.
Kwa upande wa Tanzania, hatuna kocha mzalendo wa aina ya Cisse. Kocha ambaye amekulia kwenye nchi zilizoendelea kisoka, akajifunza mpira, akaucheza na baada ya kustaafu akausomea na kuanza kuutumikia kama mwalimu. Hatuna pia kocha mzalendo aliyewahi kucheza soka la kiwango cha juu kufikia kucheza Kombe la Dunia.
Tunategemea kupata maendeleo ya kisoka kupitia walimu wa kigeni. Tunafanya hivyo wakati tukijua ripoti zote za Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) zilizotoka baada ya mashindano ya Kombe la Dunia mwaka 2010 zilizofanyikia Afrika Kusini, zilisema Afrika itaendelea kisoka kwa kuwatumia makocha wake wazalendo.
Msingi wa hoja hii ni mmoja tu; washindi wa Kombe la Dunia. Katika historia yote ya Kombe la Dunia tangu mwaka 1930, hakuna timu iliyowahi kutwaa ubingwa ikiwa na kocha wa kigeni. Mara zote kocha huwa ni mzalendo.
Kati ya mwaka 2006 hadi mwaka 2010 wakati Misri ikitwaa ubingwa wa Afrika mfululizo, kocha wake alikuwa mzalendo, Hassan Shehata. Afrika hutokea kocha mgeni akatwaa ubingwa lakini hata katika AFCON hii, nataraji bingwa atatokana na nchi inayofundishwa na kocha mzalendo.
Amunike anaweza kuwa kocha mzuri tu. Lakini hazungumzi Kiswahili, lugha ambayo inazungumzwa na wachezaji wote anaowafundisha. Hajakulia Tanzania na hajui tabia fulanifulani za Kitanzania ambazo ni muhimu kwa mwalimu kuzijua wakati anapofikiria kupanga timu yake. Mara moja moja anaweza kufanya makosa ambayo pengine angekuwa Mtanzania wa kiwango asingeweza kuyafanya.
Kama kweli tunataka kufanya vizuri huko mbele, ni muhimu kama nchi tukajiwekea utaratibu wa kutengeneza makocha wetu. Kwa mfano, mtu kama Mbwana Samatta ni muhimu akatengenezwa kuja kuwa kocha mzuri wakati utakapofika wa yeye kutundika daruga.
Lakini bado kuna hazina ya wachezaji kama Haruna Moshi, Victor Costa, Mrisho Ngassa, Kally Ongala na wengineo ambao wamewahi kwenda nje ya nchi na kupata uzoefu. Tofauti yao kubwa na Samatta ni kwamba yeye amepata uzoefu wa AFCON na ni wazi anakwenda kucheza kwenye ligi kubwa ya Ulaya hivi karibuni.

Benchi la Ufundi tena
Nimewahi kuishi Uganda kwa zaidi ya mwaka mmoja na kusema kweli kidogo nina mahaba na taifa hilo. Pasipo shaka yoyote, nitakuwa nafuatilia matokeo ya timu hiyo wakati wa AFCON. Usisahau kwamba timu hiyo ina mchezaji aitwaye Emmanuel Okwi, ambaye amenipa starehe sana kama shabiki kwenye miaka yake ya utumishi klabu ya Simba.
Wiki hii niliangalia orodha ya majina ya wanaokwenda Misri na nikavutiwa na benchi lao la ufundi. Zaidi ya Kocha Mkuu na Msaidizi wake, Uganda Cranes ilikuwa na watu ambao hawapo kwenye benchi la ufundi la Taifa Stars.