Kenya imepata pigo baada ya beki Onyango kuikosa Algeria

Muktasari:

Joash Onyango, mwenye umri wa miaka 26, aligonga vichwa vya habari baada ya picha zake kusambaa akiwa na Ndevu nyeupe, aliumia kifundo cha mguu jana jioni, katika mazoezi ya mwisho ya Stars.

Cairo, Misri. Zikiwa zimesalia saa chache kabla timu ya Kenya, Harambee Stars ijitose uwanjani kucheza mchezo wake wa kwanza, kwenye fainali za mataifa ya Afrika (Afcon), iliyoingia siku ya tatu huko Misri, habari mbaya ni kwamba, Kenya itamkosa beki wake kisiki, Joash Onyango.

Kwa mujibu wa taarifa ya uhakika iliyoifikia Mwanaspoti ni kwamba, beki huyo wa Gor Mahia aliyegonga vichwa vya habari baada ya picha zake kusambaa akiwa na ndevu nyeupe, hatocheza mchezo wa leo dhidi ya Algeria, baada ya kuumia jana jioni, katika mazoezi ya mwisho ya Stars, kabla ya mechi ya leo.

Kuumia kwa Onyango, aliyechukua nafasi ya Brian Mandela, aliyeumia wiki moja iliyopita, timu ikiwa kambini huko Paris, ni pigo kubwa kwa Kocha Sebastien Migne ambaye sasa inabidi arudishe imani yake kwa David Owino 'Calabar' na Philemon Otieno, kujenga ukuta wa ulinzi wa Kenya.

Hii inaiacha Kenya katika wakati mgumu, kwani mbali na kukosekana kwa Mandela aliyefanyiwa upasuaji juzi, Kenya pia huenda ikamkosa beki wa kati Musa Mohammed, ambaye mpaka sasa anapambana kupona jeraha alilolipata kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Madagascar, na uhakika wa kucheza leo ni mdogo.

Kwa mujibu wa ripoti ya awali kutoka kwa madaktari wa timu ni kwamba, Jeraha alilolipata Joash huenda ikamuweka nje kwa muda wa wiki mbili, hivyo atakosa mechi zote za makundi dhidi ya Algeria (leo), Tanzania (Juni 27) na Senegal Julai mosi.

Mbali na Calabar na Otieno, huenda Migne akawageukia nahodha wa U23, Joseph Okumu, na beki wa Vihiga United, Bernard Ochieng kuimarisha ulinzi wa Stars. Kabla ya bundi huyu kutua katika kambi ya Stars, Migne alikuwa anapendelea Musa na Mandela, huku Joash akiingia kutokea benchi.

SILAHA YA STARS

Katika mechi zote ambazo Stars imecheza chini ukufunzi wa mfaransa Sebastien Migne, ikiwemo mechi za kusaka tiketi ya kwenda Cairo, Silaha kubwa ya Stars, ilikuwa ni beki, ambayo ilisimama imara na kuruhusu kufungwa mara moja tu.