Kotei aishangaza Simba kumpotezea

Wednesday June 19 2019

Mwanaspoti, Michezo, Michezo blog, Mwanasport, Kotei aishangaza Simba, kumpotezea Yanga

 

By Thobias Sebastian

Dar es Salaam. Klabu ya Simba imeendelea na utaratibu wa kutangaza majina ya wachezaji waliotia saini mikataba ya nyongeza, lakini hadi sasa jina la kiungo Mghana, James Kotei halimo.

Kotei aliyecheza kwa kiwango bora katika Ligi Kuu Tanzania Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika, ameibua mjadala baada ya pande mbili za benchi la ufundi na uongozi kuvutana kuhusu usajili wake.

Usajili wa kiungo huyo mkabaji, umewagawa viongozi wa Simba ambao wapo wanaotaka apewe nyongeza ya mkataba na wengine wanataka afungashiwe virago huku Kocha Patrikc Aussems akibaki njia panda.

Akizungumza kutokea Ghana, Kotei alisema hana mawasiliano na kiongozi yeyote wa Simba na hajui hatima yake kwa kuwa mkataba wake umemalizika.

Kotei alisema mpaka anaondoka nchini baada ya msimu kumalizika hakuna mazungumzo yaliyofanyika kuhusu mkataba mpya.

Alisema baada ya kusubiri kwa muda mrefu kauli ya Simba, amejiweka sokoni kwa kutoa mwaliko kwa klabu yoyote inayomtaka kwenda kuzungumza naye. “Kabla sijasaini mkataba na timu ambayo itanitaka nitawasiliana na Simba ambao kama wataendelea kuwa kimya nitafanya uamuzi wa kutia saini na kuanza maisha mapya msimu ujao.

Advertisement

“Timu zipo nyingi zimeonyesha nia ya kunitaka, lakini nimeshindwa kufanya uamuzi kusubiri kwanza Simba kwasababu nimeishi nao vizuri kwa muda mrefu na sitaweza kufanya maamuzi magumu dhidi yao bila kunipa baraka,” alisema Kotei.

Kiungo huyo alisema anaendelea kufanya mazoezi binafsi ya viungo na ufukweni ili kujiweka fiti kwa maandalizi ya msimu ujao ingawa hadi sasa hajui atacheza timu gani.

Kotei ni mchezaji anayepambana ndani ya uwanja na amekuwa akilinda vyema safu ya ulinzi kwa kuifanya iwe salama jambo ambalo limeifanya Simba kuwa moja ya timu ngumu kufungika katika mashindano msimu uliopita.

Advertisement