Hii imekaje Neymar anaingia, Pogba aondoka Manchester United

Muktasari:

Kwa kifupi tu, Woodward hamhitaji Pogba awe bora uwanjani ndio awe kwenye kikosi cha Man United, anamtaka staa huyo aendelee kubaki Old Trafford kwa sababu moja tu ya kibiashara.

LONDON, ENGLAND. UMESHASIKIA habari za Paul Pogba. Mwenyewe anataka kubadili upepo, akisema anataka changamoto mpya. Kwa lugha nyepesi anataka kuachana na Manchester United, akajaribu maisha kwingineko.
Kocha wake huko Man United, Ole Gunnar Solskjaer ameshamchoka na anachotaka staa huyo apigwe bei tu, ili asajili wachezaji wapya watakaomsikiliza na kuitumikia timu kwa moyo.
Lakini bosi kubwa kwenye kikosi hicho, Ed Woodward hataki kusikia suala la Pogba anaondoka kwenye kikosi hicho. Sababu kubwa za Woodward ni hawezi kumuuza mchezaji ambaye anaifanya Man United kuwa imara kwenye soko la kunasa dili za kibiashara.
Woodward aliwahi kusema Man United imemaliza nafasi ya sita Ligi Kuu England msimu uliopita, kisha ikiuza mastaa wake wenye majina makubwa hapo itaonekana kama vile timu hiyo imeshuka thamani yake.
 Kwa kifupi tu, Woodward hamhitaji Pogba awe bora uwanjani ndio awe kwenye kikosi cha Man United, anamtaka staa huyo aendelee kubaki Old Trafford kwa sababu moja tu ya kibiashara.
Woodward baada ya kusikia maneno ya Pogba mwenyewe anatamani kwenda Real Madrid, basi akaamua kumthaminisha mchezaji huyo kama kuna timu inahitaji huduma yake, basi lazima ije na Pauni 150 milioni mezani, ndio mazungumzo yaanze.
Ada hiyo inaonekana ni mlima mrefu kwa Madrid na Juventus zinazomtaka. Lakini, ujanja wa Woodward ni anaamini Pauni 150 milioni zikitoka, atakuwa na uwezo wa kuingia sokoni kunasa staa mwingine atakayeifanya Man United kuwa na thamani yao kubwa sokoni.
Sasa Woodward amepata habari njema PSG inampiga bei supastaa, Neymar baada ya kuchoshwa na ustaa wake uliopitiliza.
Mabingwa hao wa Ufaransa wapo tayari kuachana na mchezaji huyo waliyemsajili kwa Pauni 198 milioni aondoke zake dirisha hili.
Gazeti moja la Ufaransa, L’Equipe limeripoti Mbrazili huyo atapigwa bei kama PSG itapokea ofa inayoendana na mipango yake.
Taarifa hizo zimekuja baada ya Rais wa PSG, Nasser Al’Khelaifi  kutaka kuwaondoa wachezaji wanaojiona ni mastaa wa kupitiliza klabuni.
Dirisha hili, Neymar amehusishwa na timu nyingi ikiwamo Madrid na Barcelona. Lakini, huko nyuma Man United ilihusishwa pia kuwa na mpango wa kumnasa staa huyo na pengine hilo italifanya wakati huu ambao inaamini kikosi chake kinahitaji mtu wa kuwafanya kuwa imara kwenye soko la kibiashara katika kipindi ambacho Pogba anataka kuondoka zake.
Man United inaamini kuwa na saini ya Neymar si tu itaifanya kuwavutia wadhamini mbalimbali, pia itaweka urahisi kwenye timu hiyo kunasa mastaa wengi wa maana ambao watahitaji kwenda kucheza timu moja na supastaa huyo wa Kibrazili.
Woodward akipata uhakika wa kumnasa Neymar, basi ni dhahiri kabisa anaweza kumfungulia milango ya Pogba kuondoka kwenye timu hiyo na kupisha ingizo jipya huko Old Trafford ambalo limezingatia zaidi kuleta wachezaji vijana wenye vipaji.
Neymar kwa sasa anauguza maumivu ya enka yanayomfanya akose michuano ya Copa America inayoendelea huko kwao Brazil.
PSG inaonekana kumchoshwa na mambo yake, ikiwamo mtafaruku mkubwa aliosababisha kwenye vyumba vya kubadilishia nguo akitibuana na wenzake, akiwamo Kylian Mbappe.
Kampuni ya CIES Football Observatory, inayojishughulisha na mambo ya kuchambua na kutathmini thamani za wachezaji, imeripoti thamani ya Neymar kwa sasa ni kati ya Pauni 107 milioni na Pauni 134 milioni, kiwango cha pesa ambacho kipo ndani ya dau ambalo Man United inamuuza kiungo wake, Pogba, anayesakwa na miamba wa Italia Juventus na wababe wa Hispania Real Madrid kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi, kwa ada ya uhamisho ya Pauni 150 milioni.