Laki za Wabongo zimefichwa benki na kina Diamond, Ali Kiba, MO Dewji

Sunday June 16 2019

 

By Luqman Maloto

UNAJUA nini? Alhamisi si ndio Serikali ya mtu mzima Magu ilituhabarisha kuhusu Bajeti mpya 2019-2020? Bajeti ilisomwa mchana. Asubuhi yake, Waziri wa Mapene, Dk Philip Mpango, alisoma “Hotuba ya Hali ya Uchumi”. Hapo ndipo topic ilipo.
Dk Mpango kama jina lake ni mtu wa mipango. Wizara anayoiongoza inahusu mipango ya mikwanja. Katika hotuba hiyo, Mpango aliwagusa Wabongo kumoyo aliposema pato la Mbongo kwa mwaka 2018, liliongezeka kwa kilo moja, yaani Sh100,000.
Watu wanalalamika usawa wa Dk Magu unakaba, vyuma vinakaza, halafu unawaambia kipato chao kimeongezeka kwa laki-laki. Basi, tangu hiyo taarifa itoke watu wamekimbilia benki kuchungulia kama laki zimeingia bila wao kujua. Wapo wamezisaka kwenye simu. Wengine wamepekua vyumbani wanatafuta laki hadi uvunguni.
Ukikatiza mtaani unaambiwa “wanatuongopea mbona laki hazipo!” Ni hivi; Wabongo wanasema vipato vyao havijaongezeka kwa laki-laki. Wengine wanalalamika hela zimepungua, halafu wanaliwazwa mchana kweupeee kuwa wameongeza laki-laki.
Mimi nawajibu hivi; Wabongo laki-laki zao kweli zipo. Sema nini? Zimefichwa benki na kina Ali Kiba, Harmonize, Diamond Platnumz, MO Dewji, Rostam Aziz, Said Bakhresa na wengine kibao.
Naomba nifafanue; kuna watu wachache Bongo wana mkwanja mreeefu! Hao ndiyo wanafanya mamilioni ya Wabongo waonekane wamezidisha laki-laki kwenye vipato vyao, wakati kwa hali halisi wala hawazioni.

BADO UPO GIZANI?
Alichokisema Mpango ni kitu ambacho wachumi wanakiita GDP per capita. Ukishapata unyama kamili wa hicho kitu, ndipo utaelewa kwa nini Mwashilona wa Mbalizi anaambiwa ana laki imeongezeka wakati yeye mwenyewe haioni. Kumbe Nandy kaziweka hizo hela benki kwa niaba yake.
Kuinyaka GDP per capita, sharti kwanza uitambue GDP. Kwa kifupi GDP ni Pato la Taifa. Ufafanuzi, ni kipimo cha thamani ya fedha kwenye soko la nchi. Ule mzunguko wa kifedha katika kuuza na kununua ndani ya nchi ndio Pato la Taifa.
GDP per capita ni ile jumla ya fedha (Pato la Taifa) gawia kwa idadi ya watu wote kwenye nchi. Matokeo hayo husababisha asiye na mchango kwenye mzunguko wa fedha kwenye nchi, apimwe sawasawa na wale wenye kuzungusha noti nyingi.
Yaani Shinyuni wa Malampaka anapimwa sawa na Rostam. Matokeo hayo, mtu ambaye ameongeza mabilioni, naye anahesabiwa ameongeza laki. Yule ambaye yeye amefilisika na kukimbia mji, anahesabiwa kaongeza laki. Mfungwa gerezani naye anasemwa kaongeza laki.
Hivyo, wakati wowote ukiona GDP per capita imeongezeka halafu wewe unapigika, ujue kuna watu wamepiga hela ndefu na zimeonekana kwenye mzunguko wa Pato la Taifa, kwa hiyo wamekubeba uonekane nawe umo, lakini huna ujanja wa kuzichukua. Zipo kwenye akaunti zao.
Inawezekana pia ukawa unatengeneza mahela mengi halafu unaambiwa kipato cha kila Mtanzania hakijaongezeka au kimeshuka, hapo utambue kuna watu kibao hawazalishi, hivyo wamekufanya na wewe uonekane umepigika kama wewe.
Hata hii taarifa ya laki-laki wewe ukimaindi wamesema umezidisha laki wakati huna, jiulize MO akimaindi naye itakuwaje? Biashara zake, ajira alizotoa, mishahara anayolipa, halafu anaambiwa mwaka mzima 2018 aliongeza kipato cha laki tu.
Mpango alisema, mwaka jana Pato la Taifa lilikuwa Sh129.4 trilioni na watu walikadiriwa kuwa 52 milioni. Hivyo, ukigawa Sh129.4 trilioni kwa watu 52 milioni, unapata Sh2.4 milioni, wakati mwaka 2017, ilikuwa Sh2.3 milioni. Hapo ndipo akasema, laki imeongezeka kwa kila kichwa.
Wakati Mpango akisema hivyo, ripoti ya Forbes imeonyesha kuwa utajiri wa MO umeongezeka kutoka Dola 1.5 bilioni mwaka 2017 mpaka Dola 1.9 bilioni mwaka jana. Ongezeko la Dola 4 bilioni kwa chenji ya Kibongo ni kama Sh9.2 trilioni. Halafu anaambiwa na yeye ameongeza laki tu mwaka jana, sawasawa na Mfutulio wa Nyang’wale ambaye mwaka mzima hakukamata hata tembo mwekundu mmoja.
Mwaka jana Diamond Platnumz alinunua mjengo wa kibingwa sana Mbezi Beach, Harmonize hakamatiki kwa matumizi, ana pesa mpaka kila wakati anajihisi zinamuwasha, Ali Kiba ni tajiri hadi akawa mdhamini wa klabu ya Ligi Kuu Bara, Coastal Union. FA na manukato yake anayoendelea kuyauza.
Fid Q walimtibua kidogo kuwa hana hela wala gari, basi akaamua kwa hasira kushusha Jeep la bei mbaya. AY na michongo yake, Ommy Dimpoz mwenye ziara nyingi za Ulaya na Marekani. Eti wote hao wanasemwa waliingiza laki-laki sawasawa na Tumfyule wa Kazuramimba ambaye laki hajui inafafanaje.
Sasa unakaa unanuna umesingiziwa laki imeongezeka kwako wakati huna kitu, jiulize na wabunge wanaopokea mamilioni kila mwezi, lakini nao wanahesabiwa wamekichanga kwa nyongeza ya laki mwaka mzima. GDP per capita ni wastani. Wenye kikubwa, walio na kidogo, vilevile wasionacho, wanapimwa sawa.

UTAELEWA HII KITU
Usimnunie Mpango wala usimdai, komaa na kina Ali Kiba. Sekta ya sanaa na burudani imezifundisha adabu nyingine nyingi mwaka 2018. Kwa maana hiyo, kama watu hawakuona pesa katika biashara zao, wajue kina Vanessa Mdee walinyoosha sana.
Dk Mpango alisema, shughuli za sanaa na burudani ziliongoza mwendo kukua kwa kasi ya asilimia 13.7. Ujenzi ilikamata namba mbili kwa kukua asilimia 12.9. Uchukuzi na uhifadhi mizigo asilimia 11.8. Shughuli za kitaaluma, sayansi na ufundi asilimia 9.9. Habari na mawasiliano asilimia 9.1. Kilimo asilimia 5.3.
Maana yake sanaa na burudani kwa jumla ilitengeneza fedha ndefu mwaka jana. Hapo ndio maana unawaona majanki kama Harmonize, wananunua vitambulisho vingi vya wajasiriamali a.k.a vitambulisho vya Magufuli. Halafu wanakwenda kugawa bure kwa wamachinga.
Unajiuliza wametoa pesa wapi? Hayo ndiyo matokeo yenye kuonekana, burudani ina pesa nyingi. Inakua kwa kasi kubwa kuliko sekta mama kwenye nchi ambayo ni kilimo. Wenye burudani ndiyo hao, unashangaa vipi sasa kuwaona kina Aslay wanakokota BMW? Unastaajabu nini majanki kusafiri kwa Emirates business class?
Sasa wakati burudani ikitengeneza mapene ya kutosha, kuna sekta zinajifia, watu kibao wamepoteza ajira. Unakuta mahela ya Jux yamesababisha wale wasio na ajira ambao wametoka afadhali mpaka sifuri, lakini wanasomeka wana laki-laki kwa kuwakadiria kutoka kwenye Pato la Taifa.
Mimi mwenyewe baada ya kuambiwa nimeongeza kipato cha laki, nimekuwa nikiwaza itakuwa laki yangu imesoma kwa Bakhresa au MO? Ila sio kesi, siku nikikutana na Ally Mufuruki, nitamtaiti anipe laki yangu, itakuwa imesomea kwake.
Piga kazi mwana. GDP per capita ni kipimo tu cha mzunguko wa fedha kwenye nchi, kama huna ujue huna. Komaa ili uwabebe wenzako na sio ubebwe. Ukubwa wa GDP per capita ni ishara ya ukuaji mzuri wa kiuchumi.

Advertisement