Lazio yajitosa kwa Samatta yamtegea Sh40 bilioni

Sunday June 16 2019

Mwanaspoti, Lazio yajitosa kwa Samatta, yamtegea Sh40bilioni, Mwanaspoti, Michezo blog, Michezo

 

Roma, Italia. Miamba ya Italia, SS Lazio imejitosa katika mbio za kumwanua mshambuliaji wa Tanzania na KRC Genk, Mbwana Samatta kwa dau la euro 16milioni (zaidi Sh40 bilioni).

Kwa mujibu wa mtandao wa klabu hiyo, Lazio imemuweka Samatta katika orodha ya nyota inayowasaka kupitia dirisha la majira ya joto, ikielezwa imemtengea kasi cha Euro 16 milioni (zaidi ya Sh 40 bilioni), ikiwa ni kiwango cha juu kuliko kilichotajwa kutaka kutolewa na klabu za England.

Klabu za Aston Villa, Watford, Leicester, Brighton na Burnley zote zimekuwa zikitajwa kuwinda saini na nyota huyo wa kimataifa wa Tanzania anayekipiga Genk ya Ubelgiji zikichuana na AS Roma ya Italia pamoja na Olympique Lyon ya Ufaransa.

Hata hivyo, Lazio walioshika nafasi ya nane katika Serie A msimu uliopita nao wameingia kwenye mbio hizo za kumnasa straika huyo aliyeifungia Genk mabao 23 na kuiwezesha kubeba Ubingwa wa Ligi Kuu ya Ubelgiji na kukata tiketi ya Ligi ya Mabingwa ya Ulaya.

Samatta aliyesajiliwa Genk kutoka TP Mazembe ya DR Congo mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2021 kwa sasa yupo Misri akijiandaa kuiongoza Tanzania kwenye mechi za Fainali za Afcon 2019 zitakazofanyika kati ya Juni 21 hadi Julai 19.

Tanzania imepangwa kundi C sambamba na Senegal, Algeria na Kenya na usiku wa jana ilikuwa uwanjani kucheza mchezo wao wa pili wa kujipima nguvu dhidi ya Zimbabwe baada ya awali kufungwa bao 1-0 na Italia wiki iliyopita jijini Cairo.

Advertisement

Kujitokeza kwa Lazio kunaifanya klabu hiyo kuchuana na majirani zao wa Roma iliyoanza mapema harakati za kuisaka saini ya nyota huyo wa zamani wa Simba, japo mwenyewe amekuwa akisisitiza anatamani mno kucheza soka England kama ataondoka Ubelgiji.

Advertisement