Zainabu Kiba: Nimemtuliza Banda na maumivu ya Kocha Amunike

Muktasari:

Ndio, mke wa Banda anayekipiga Baroka FC ya Afrika Kusini, Zainabu Kiba anamtuliza staa huyo anapokuwa kwenye ‘mudi’ mbaya kwenye kazi yake ya soka ama maisha ya kawaida tu.

UKISIKIA tulizo la moyo usidhani ni Panadol ama ndumba kwa waganga aisee. Kila mtu ana tulizo la moyo wake, yaani mtu ambaye hutuliza maumivu ya mwingine.

Ndivyo ilivyo kwa staa wa kimataifa wa Tanzania, Abdi Banda, ambaye anapopatwa na majanga basi akirejea nyumbani hukutana na tabasamu la Zabibu na hapo moyo wake hutulia tuliiii.
Ndio, mke wa Banda anayekipiga Baroka FC ya Afrika Kusini, Zainabu Kiba anamtuliza staa huyo anapokuwa kwenye ‘mudi’ mbaya kwenye kazi yake ya soka ama maisha ya kawaida tu.
Mwanaspoti lilianza na tukio la Banda kutemwa Taifa Stars kinachoshiriki michuano ya AFCON na hapa Zabibu anafunguka mwanzo mwisho.
“Nilipoona hilo nikampigia simu kwa sauti ya mahaba, nikamjulia hali nilipoona yupo kwenye ari ya kunielewa nikamwambia ujue mume wangu wewe ni bonge la mchezaji, weka bidii utafika mbali, akacheka akasema haina neno.
“Haikuwa nafasi yako kushiriki Afcon so amini bado una nafasi ya kuitetea nchi yako katika mashindano mengine hivyo, rudi ujipange upya,” hayo ni maneno ya Zabibu kwa Banda.

ISHU YA BANDA IPO HIVI
Baada ya Banda kutemwa Taifa Stars, maneno mengi yakaibuka huku wengine wakidai kiwango kimeshuka, basi unambiwa Zabibu hakutaka kulifumbia mdomo hilo akaeleza kuwa, sababu kubwa ni beki huyo kukaa nje ya nje muda mrefu.
“Sifuatilii sana mambo ya soka kwa sababu mume wangu hapendi, lakini suala la kushuka kiwango hilo sio kweli kabaisa. Ameshindwa kufanya vizuri inaweza kuwa sababu ya kukaa nje kwa muda mrefu akiwa majeruhi.
“Alikuwa nje ya uwanja kwa miezi minne na alikuwa ni mtu wa nyumbani na hilo inaweza kuwa sababu ya kuyumba kwake. Watanzania wampe muda atarejea kwenye kiwango chake na kuitumikia Taifa Stars na klabu yake ya Baroka,” alisema Zabibu.

HASIRA ZA
BANDA ZATULIZWA
Kwa wapenzi wa soka hakuna asiyefahamu hasira za Banda pale anapofanyiwa tukio lisilo la kiungwana uwanjani au walinzi wenzake wanapofanya makossa, amekuwa akionyesha hasira jambo ambalo Zabibu amebainisha kuwa sio uwanjani tu hata nyumbani.
“Banda ana hasira ila najua namna ya kumkabili akiwa katika hali hiyo. Huwa hapendi kuzungumza akiwa na mudi hiyo hivyo, namuacha na baada ya hapo nakaa naye ili kurudisha furaha yake.
“Huwa hana nafasi ya kucheka muda mrefu nikimpa maneno mazuri nikitaka kujua kama amenielewa basi huwa naangalia sura yake tu,” alisema Zabibu.