Bocco amekuwa mtamu kila uchwa mjue

Muktasari:

Ukiachana na hilo msimu uliomalizika unakuwa wa 11 kwa Bocco akicheza Ligi Kuu Bara akiwa na timu mbili tofauti, Azam FC aliyoitumikia kwa miaka tisa kisha Simba ambayo msimu ujao utakuwa wa tatu kwake.

DAR ES SALAAM.ACHANA na ile ishu ya kusaini Polokwane ya Afrika Kusini. Mabosi wa Simba hawana presha  wanashusha majembe mapya na kuongeza nguvu.
 Msimu ujao Simba itashiriki mashindano ya ndani pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika, ni lazima iwe na watu wa kazi.
Katika kuhakikisha inakuwa na kikosi imara, Simba ikatumia akili nyingi kwa kuwabakiza kikosini mastaa wake walioibeba msimu uliopita na hatimaye kuipa taji la Ligi Kuu Bara kwa mara ya pili mfululizo na kuifikisha hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Miongoni mwa mastaa waliobakizwa kikosini hapo ni nahodha, John Raphael Bocco, ambaye baadaye taarifa zilivuja kuwa amemwaga wino Polokwane City.
Ukiachana na hilo msimu uliomalizika unakuwa wa 11 kwa Bocco akicheza Ligi Kuu Bara akiwa na timu mbili tofauti, Azam FC aliyoitumikia kwa miaka tisa kisha Simba ambayo msimu ujao utakuwa wa tatu kwake.
Septemba 24, 2008, John Bocco alifunga bao lake la kwanza Ligi Kuu Bara wakati Azam FC iliposhinda 2-0 dhidi ya Toto African ya Mwanza, ambayo ilishuka daraja msimu wa 2015-16.
Mwanaspoti lilikufichulia rekodi za Bocco kwa mara ya kwanza msimu uliopita, ambapo alimaliza akiwa na mabao 14 huku akifikisha mabao 98 kwa muda wote wa misimu 10 aliyokipiga.
Makala haya ni mwendelezo wa rekodi za Bocco ambazo ameziweka Ligi Kuu Bara tangu ameanza kucheza soka la ushindani mwaka 2008, akiwa na kikosi cha Azam ambacho ndicho alichokitumikia kwenye msimu wake wa kwanza.

REKODI ZA BOCCO
-Amecheza Azam misimu 9.
-Amecheza Simba misimu 2.
-Ameongeza mkataba Simba wa miaka 2.
-Mkataba wake wa kwanza na Simba ulikuwa na thamani ya Sh 30 milioni.
-Mshahara wa mkataba wake wa kwanza ulikuwa Sh 2 milioni.
-Amecheza Ligi Kuu Bara akiwa na timu mbili Azam miaka 9.
-Simba miaka 2 na ameongeza mkataba wa miaka 2.
-Amefunga jumla ya mabao 114
-Akiwa Azam amefunga mabao 84.
-Akiwa Simba amefunga mabao 30.
-Bocco amewahi kushinda tuzo mbalimbali kwenye ligi, Kiatu cha Dhahabu (Mfungaji Bora) alichoshinda msimu wa 2011-12 alipomaliza ligi akiwa na mabao 19.
-Msimu uliopita 2017-18 alishinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi.
-Msimu uliopita 2017-18 alishinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa Simba.
-Msimu huu 2018-19 ameshinda Tuzo ya Mshambuliaji Bora wa Simba.
-Bocco amefunga mabao matatu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ulioisha.