Mo Dewji aivamia AS Vita kibabe

Sunday June 16 2019

kuivamia kibabe AS Vita, Simba kuna majina, wachezaji zaidi ya 30

 

By THOBIAS SEBASTIAN

Dar es Salaam. KAZI ndio imeanza na mabosi wa Simba wamekutana kimyakimya kupanga mikakati ya kushusha majembe mapya na tayari wameingia kwenye rada za wakali wawili wa AS Vita ya DR Congo.
Kwanza, mfadhili wao, Mohammed Dewji ‘Mo alianza kuwasainisha mikataba mipya mastaa wa kikosi cha kwanza na sasa wamehamia anga za kimataifa ili kusuka kikosi kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kama ambavyo Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori alitangaza kuwa watafanya usajili wa kishindo ndani ya siku 10 zijazo, ndio wameanza kuonyesha jeuri ya pesa kwa kuivamia kibabe AS Vita ambayo walichuana nayo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita.
Mwanaspoti linafahamu kuwa katika vikao vya mabosi wa Simba kuna majina ya wachezaji zaidi ya 30 ambayo yatachambuliwa ili kupata sura za kazi kwa ajili ya kuwababa mabingwa hao kwenye anga za kimataifa.
Miongoni mwa majina hayo yapo ya mabeki wawili wa kushoto na wa kati wa AS Vita ambao tayari Kocha Patrick Aussems amewapendekeza wawepo kwenye usajili wa msimu huu.
Mabeki hao ni Yannick Bangala Litombo na Gladi Ngoda Muzinga ambao wote walicheza mechi dhidi ya Simba.
Iko hivi, Aussems katika ripoti yake ya msimu huu kwenye usajili anataka kusajiliwa kwa wachezaji wanne wa kigeni ambao ni straika wenye uwezo wa kushambulia kutoka pembeni ama katikati. Hatua hiyo inalenga kuhakikisha msimu ujao Simba inafunga idadi kubwa ya mabao na hata kama itamkosa Emmanuel Okwi, basi kusiwe na pengo.
Pia, anahitaji kiungo wa kati mwenye uwezo wa kukaba na kushambulia ili kusaidiana na Jonas Mkude kwani James Kotei hakuna uhakika kama atakuwepo msimu ujao. Kwa sasa Kotei yupo kwao Ghana na hajasaini mkataba mpya.
Mchezaji mwingine ni beki wa kati na hapo pendekezo la Aussems likatua kwa Litombo, ambaye alimfuatilia tangu Simba ilipovaana na AS Vita kwenye mchezo wa kwanza hadi ule wa marudiano.
Litombo anamvutia Aussems kwani anaweza kumtumia kama mbadala wa Juuko Mushid, ambaye huenda akatemwa msimu ujao.
“Tunaendelea kupitia vielelezo vya kila mchezaji ili kujua ambaye tutamsajili kama atakidhi mahitaji ya mwalimu ili kutimiza malengo ya timu msimu ujao,” alisema mmoja wa viongozi wa juu ambaye aliomba jina lake lisitajwe gazetini.
 
MSIKIE AUSSEMS
Aussems ambaye yupo likizo nchini Ubelgiji, alisema tayari ameshamaliza masuala ya usajili kwa kuwapa viongozi mahitaji yake na kila sehemu ambayo anataka iongozewe nguvu kwa kuweka chaguo la kwanza hadi la tatu. “Kipindi cha usajili kuna wachezaji wazuri ambao tunawahitaji, lakini pia wanatakiwa na timu zingine, hivyo zoezi linafanyika kwa usiri na umakini wa hali ya juu ili kukamilisha mahitaji.
“AS Vita kuna wachezaji wazuri na tuliwaona wakati tunacheza nao waliokuwa bora na wapo ambao wanafaa kuichezea Simba.
“Tunafanya kazi kwa kuwasiliana na uongozi na kazi inaendelea vizuri kwani, miongoni mwa mapendekezo waliyofanyia kazi ni eneo la kipa kwa kumsajili Benno Kakolanya, ambaye naamini ni miongoni wa wachezaji bora,” alisema Aussems
“Wachezaji ambao watasajiliwa nina imani ni wazuri kama ilivyo kwa Litombo na Muzinga.
 
 MSIKIE MAGORI
Mtendaji Mkuu wa Simba, Magori ambaye juzi alitangaza kuachia ngazi baada ya mkataba wake kumalizika huku akitumikia kwa siku 60 zijazo, alisema wanaendelea na harakati za usajili.
Kuhusu Litombo alisema ni miongoni mwa wachezaji waliotajwa na Aussems, lakini hapo awali walishindwa kukamilisha dili kutokana na AS Vita kutaka walipwe Dola 150,000 (Sh400 milioni).
“Hiyo pesa tungeilipa AS Vita tu na hapo bado mchezaji mwenyewe angeweka masharti yake, lakini kwa sasa lolote linaweza kutokea.
“Si Litombo tu ambaye atasajiliwa na Simba kwa ajili ya msimu ujao. Kama Bodi tunaendelea kuchuja wachezaji ili mwalimu akidhi mahitaji yake,” alisema.
 
Simba yampa mtihani Bwalya
Wakati huohuo taarifa kutoka Zambia zinasema Wekundu hao wapo katika hatua ya kumsajili mshambuliaji Walter Bwallya, lakini straika huyo amepewa kazi moja nzito.
Simba ilijaribu kuongea na Nkana Rangers ya Zambia juu ya kutaka kumsajili Bwalya, lakini Wazambia hao wakahitaji fedha nyingi.
Akili ya Simba inaelezwa wamekubaliana kila kitu na Bwallya lakini wamemtaka mshambuliaji huyo kutafuta njia ya kuachana na klabu yake ili avae jezi ya Simba kwa msimu ujao.

Advertisement