Kakolanya atia kibindoni Sh45 milioni za Simba kama utani vile

Muktasari:

Kakolanya aliyekuwa kipa namba moja kwenye kikosi cha Kocha Mwinyi Zahera alishindwa kumalizia msimu huo kutokana na kuenguliwa kwenye kikosi baada ya kugoma kufanya kazi akidai mishahara na pesa ya usajili

KIPA Beno Kakolanya amesaini mkataba wa miaka miwili wa kuitumikia klabu ya Simba kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa.
Kama ambavyo Mwanaspoti lilikutonya miezi kadhaa iliyopita wakati Kakolanya aliyekuwa anaichezea Yanga msimu uliopita, alipoingia kwenye mgogoro mzito na waajiri wake, tayari ametua Msimbazi.
Kakolanya aliyekuwa kipa namba moja kwenye kikosi cha Kocha Mwinyi Zahera alishindwa kumalizia msimu huo kutokana na kuenguliwa kwenye kikosi baada ya kugoma kufanya kazi akidai mishahara na pesa ya usajili. Baada ya kukaa nje ya uwanja mabosi wa Simba ndio wakaanza kumpigia hesabu kwa ajili ya kuimarisha kikosi na kumpa changamoto kipa Aishi Manula, baada ya Deogratius Munish ‘Dida’ kuonekana kutohimili ushindani.
Kabla ya Kakolanya kutua Msimbazi alikuwa anawindwa na Mufulira Wonderers FC pamoja na Zesco zinazoshiriki Ligi Kuu nchini Zambia, na meneja wa mchezaji huyo, Seleman Haroub alikiri mapema kupokea ofa hizo.
Haroub alisema: “Ofa ya timu za Simba na Mufulira zipo lakini timu ambayo itafika dau basi atamalizana nayo.”
Lakini, hakuna timu yoyote ya nje ambayo iliweza kumalizana naye, ndipo kasi ya kumsajili Kakolanya kwa mabosi wa Simba iliongezeka baada ya klabu yake ya zamani (Yanga) kutoa barua ya kuvunja mkataba kwa pande mbili kukubaliana.
Mwanaspoti linafahamu kuwa mwekezaji wa Simba, Mohammed Dewji alikaa chini na kocha Patrick Aussems na kupitisha jina hilo na moja kwa moja kazi ikaachwa kwa Salim Abdallah ‘Try Again’ kumaliza mchezo.

VIPIMO USIPIME
Baada ya jina la Kakolanya kupelekwa kwa Try Again kulionekana kulikuwa na uzito wa moja kwa moja mchezaji huyo kusajiliwa bila afya yake kujulikana.
Kakolanya alifanyiwa vipimo kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili wiki mbili zilizopita, kisha akamwaga wino na mpango mzima ulifanywa kwa usiri mkubwa.
Mtu wa karibu na Kakolanya alisema ilimchukua takribani wiki mbili katika vipimo hivyo hadi mabosi wa Simba wakakubali wenyewe. “Waliangalia vipimo vyote hasa moyo, lakini goti pamoja na bega na waliridhika dogo yuko vizuri,” alisema mtu wake wa karibu.

ALAMBA MILION 45
Baada ya kukamilisha vipimo hivyo, Kakolanya aliwekewa mezani mkataba Sh30 milioni, lakini aligomea ofa hiyo.
Baada ya kugoma Try Again alirudi tena kwenye meza ya mazungumzo na Kakolanya akataka alipwe dau kubwa zaidi kwani, tayari kulikuwa na ofa tamu Zambia.
Hata hivyo, Try baada ya kushauriana na Mo, maamuzi yakafikiwa kuwa alipwe dau la Sh45 milioni kwa mkataba wa miaka miwili.
Pia, kwenye mkataba huo kuna maslahi mengine ambayo kipa huyo atakuwa akipatiwa ikiwemo nyumba ya kuishi kama alivyokuwa akifanyiwa wakati akiwa Yanga.
Kuwasili kwa Kakolanya ndani ya Simba ina maana kwamba, Deogratius Munish ‘Dida’ shughuli yake itakuwa imemalizika Msimbazi.
Pia, Kakolanya anatarajiwa kutoa upinzani mkubwa kwa Manula, ambaye amekuwa kipa namba moja pale Msimbazi kwa muda mrefu.

Mwenyewe Afunguka
Mwanaspoti lilimtafuta Kakolanya ili kuzungumzia changamoto atakazozipata Msimbazi, lakini akasema si wakati sahihi wa kueleza mikakati yake, lakini anafahamu mambo yote na ndio sababu amesaini Simba.
“Kwa sasa niko Mbeya, lakini sio sahihi kwa sasa kuzungumzia suala hilo. Fahamu kuwa hadi nakuja Simba nimeshajipanga kwa changamoto zote,” alisema.