Ronaldo azidi kumtega Messi kwa mataji ya timu ya Taifa

Monday June 10 2019

Mwanaspoti, Ronaldo, kumtega, Messi, Michezo, Mwanasport, Soka

 

By Charles Abel

Dar es Salaam. Nyota wa Ureno, Cristiano Ronaldo anazidi kumuweka kikaangoni mwenzake wa Argentina, Lionel Messi baada ya Ureno kutwaa taji la mashindano ya UEFA Nations League jana usiku.

Bao la dakika ya 60 la winga wa Valencia, Goncalo Guedes lilitosha kuipa taji Ureno mbele ya Uholanzi ambayo awali ilikuwa ikipewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa huo kutokana na kiwango bora ambacho imekionyesha kwenye mashindano hayo.

Ureno imetwaa taji hilo siku tano kabla ya kuanza kwa mashindano ya Copa America ambayo Messi atakuwemo kwenye kikosi cha Argentina kujaribu kumaliza mkosi wa kushindwa kutwaa taji lolote kikubwa akiwa na kikosi cha timu ya Taifa ya Argentina.

Vita ya ushindani baina ya wawili hao ambayo ilianzia kwenye mafanikio yao katika ngazi ya klabu imekuwa kubwa kiasi cha kuhamia hadi kwenye timu zao za taifa ambako wamekuwa wakitazamwa kama wakombozi na kubeba lawama pindi zinapofanya vibaya.

Messi ndiye amekuwa muhanga zaidi kwani kila Ureno inapofanya vyema, hujikuta akitazamwa kama mchezaji asiyetoa mchango kwa timu yake ya taifa ya Argentina kulinganisha na Ronaldo na ni wazi kwamba taji hilo ambalo Ureno wamelipata litamweka kwenye presha kubwa katika mashindano ya Copa America.

Pamoja na kutofunga bao hilo, Ronaldo ametoa mchango mkubwa kuifikisha Ureno kwenye hatua ya fainali kwani alipachika mabao matatu katika ushindi wa mabao 3-1 ambao nchi hiyo iliupata dhidi ya Uswizi kwenye mechi ya nusu fainali.

Advertisement

Hata hivyo mashindano hayo ya UEFA Nations League hayatofanyika tena na badala yake, Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA) limeamua kuendelea na mashindano yake ya EURO.

Advertisement