Aussems, Zahera undavaundava tu

Muktasari:

Makocha hao walionekana kufanya vizuri msimu uliopita kwa kuchuana kuwania ubingwa ambapo Yanga iliongoza msimamo kwa muda mrefu kabla ya kuja kukata pumzi mwishoni na watani wao kukalia kiti na kubeba taji kiulaini hawachekenai kwenye tuz

LICHA ya kuonyeshana kazi mwanzo mwisho kwenye Ligi Kuu Bara msimu uliopita na Simba kubeba taji kwa msimu wa pili, huku Yanga ikitoka kapa pia kwa mara ya pili mfululizo makocha wa timu hizo Mwinyi Zahera na Patrick Aussems wala hawachekani.
Ndio, Makocha hao walionekana kufanya vizuri msimu uliopita kwa kuchuana kuwania ubingwa ambapo Yanga iliongoza msimamo kwa muda mrefu kabla ya kuja kukata pumzi mwishoni na watani wao kukalia kiti na kubeba taji kiulaini hawachekenai kwenye tuzo.
Kamati ya Tuzo za Mwezi za Ligi Kuu Bara chini ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilimtangaza Aussems kunyakua tuzo ya tatu mfululizo katika ligi hiyo, lakini hiyo haijamfanya amzidi ujanja Zahera kwani kila mmoja amemaliza msimu akiwa na tuzo tatu.
Zahera aliyepo kwa sasa kwenye majukumu ya kuiandaa timu ya taifa ya DR Congo ‘The Leopards kwa fainali za Afcon 2019, ndiye aliyekuwa kochja kinara kwa kutwaa tuzo za Kocha Bora wa Mwezi akitwaa mara tatu kabla ya Aussems kupiga hat-trick yake juzi.
Makocha hao wanaweza kuendelea kuchuana msimu ujao kutokana na aina ya vikosi na wachezaji walionao, hasa baada ya Zahera kuanza mapema kuongeza majembe mapya,
ilihali Aussems akipendekeza kwa mabosi wake aongezewe vifaa vya maana ili watishe.
Mkongo wa Yanga, yeye alinyakua tuzo hizo Septemba, Novemba na Desemba, wakati Aussems ameibeba mfululizo kuanzia Machi, Aprili na Mei, huku Amri Said wa Biashara United alinyakua Agosti kipindi akiinoa Mbao FC.
Wengine walionyakua tuzo hiyo inayoambatana na kitita cha Sh 1 milioni imenyakuliwa pia na Hans Pluijm (Oktoba) kipindi akiinoa Azam FC, Etienne Ndayiragije wa KMC (Januari) na Mohammed ‘Adolph’ Rishard wa Tanzania Prisons (Februari).

KAGERE NOMA
Kwa upande wa wachezaji, straika wa Simba na Mfungaji Bora wa Ligi Kuu 2018-2019, Meddie Kagere amefunika bovu akikosa mpinzani katika tuzo za Mchezaji Bora wa
Mwezi kwa kunyakua mara tatu ikiwamo ya juzi aliyotangazwa sawia na kocha wake.
Kagere aliyesajiliwa na Simba msimu uliopita akitokea Gor Mahia ya Kenya na kuifungia jumla ya mabao 39 kwa michuano yote, ndiye aliyekuwa mchezaji wa kwanza kunyakua tuzo hiyo alipotangazwa Agosti mwaka jana.
Pia amenyakua tuzo hiyo Februari na Mei, huku straika anayeondoka Yanga, Heritier Makambo na nahodha wa Simba, John Bocco wakimfuata Kagere kwa kila mmoja kutwaa tuzo hiyo mara mbili mfululizo katika miezi tofauti.
Makambo alitwaa tuzo Novemba na Desemba, wakati Bocco alifanya hivyo Machi na Aprili, huku Eliud Ambokile aliyekuwa Mbeya City akibeba Septemba, Emmanuel Okwi
wa Simba (Oktoba), wakati Januari ilibebwa na Dickson Ambundo wa Alliance.
Kwa hesabu zilivyo za tuzo hizo, Simba ndio klabu iliyonyakua tuzo nyingi za mwezi kwa jumla wake kuliko klabu nyingine kwani imebeba tisa, huku ikifuatia Yanga ilioyotwaa mara tano, huku klabu za Mbao, Azam, KMC, Mbeya City, Alliance na Prisons zikigawa mara moja moja.

Vinara wa Tuzo za TPL 2018-2019
MCHEZAJI BORA
Agosti-Meddie Kagere (Simba)
Septemba- Eliud Ambokile (Mbeya City)
Oktoba-Emmanuel Okwi (Simba)
Novemba-Heritier Makambo (Yanga)
Desemba-Heritier Makambo (Yanga)
Januari- Dickson Ambundo (Alliance)
Februari-Meddie Kagere (Simba)
Machi-John Bocco (Simba)
April- John Bocco (Simba)
Mei- Meddie Kagere (Simba)

MAKOCHA BORA
Agosti- Amri Said (Mbao)
Septemba- Mwinyi Zahera (Yanga)
Oktoba- Hans Pluijm (Azam)
Novemba- Mwinyi Zahera (Yanga)
Desemba- Mwinyi Zahera (Yanga)
Januari- Etienne Ndayiragije (KMC)
Februari- Mohammed ‘Adolph’ Rishard (Prisons)
Machi- Patrick Aussems (Simba)
Aprili- Patrick Aussems (Simba)
Mei- Patrick Aussems (Simba)

KLABU KINARA
1- Simba SC (9)
2- Yanga SC (5)
3- Alliance FC (1)
4- Azam FC (1)
5- KMC FC (1)
6-Mbeya City (1)
7- Mbao FC (1)
8- Prisons (1)