Olunga atua Paris, tayari kuwavaa Madagascar kesho

Muktasari:

Baada ya mechi ya kesho, Stars ikiwa Kundi C pamoja na majirani zao Tanzania, Senegal na Algeria, itacheza mechi nyingine ya kirafiki itakayopigwa Juni 15, huko Madrid Hispanic, dhidi ya DR Congo.

Nairobi. Ametua mwanangu! Naam Straika timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars na klabu ya Kashiwa Reysol ya Japan, ametua Jijini Paris mapema leo na kuungana na kikosi cha Stars, tayari kuwavaa Madagascar kesho.

Awali, kulikuwa na hofu kuwa, huenda Injinia huyo angekosa mechi hiyo ya kujipima ubavu ambayo imepangwa kupigwa kesho kuanzia saa tatu usiku, ugani Stade Robert-Robin, baada ya klabu yake kudinda kumuachia kabla ya kulegeza kamba.

Olunga aliyetua Paris asubuhi, ameungana na wachezaji wengine kambini ambapo jioni hii amefanya mazoezi na timu, na kwa mujibu wa Kocha mkuu wa Harambee Stars, mfaransa Sebastian Migne, Olunga ataanzia benchi kwenye mchezo wa kesho.

"Nimefurahi sana kwa ujio wake, Olunga ni mtu muhimu, morali kambini na mazoezini kama mlivyoshuhudia jioni imeongezeka maradufu. Kwa kuwa bado ana uchovu, niweke tu kwamba, kesho ataingia kipindi cha pili," alisema Migne.

Kuhusu hali ya wachezaji kocha huyo ambaye ni kocha wa kwanza kuipeleka Kenya katika fainali hizo baada ya miaka 15, alisema mpaka sasa hakuna majeruhi yeyote na kusisitiza kuwa vijana wake wako tayari kifisikali na kisaikolojia.

Baada ya mechi ya kesho, Stars ambayo iko kundi C pamoja na majirani zao Tanzania, Senegal na Algeria, itacheza mechi nyingine ya kirafiki itakayopigwa Juni 15, huko Madrid Hispanic, dhidi ya DR Congo.

Kenya, itaanza kutupa karata yake Juni 23, dhidi ya Algeria, kisha itavaana na Tanzania (Juni 27) kabla ya kumalizana na Senegal, Julai Mosi. Mechi zote zitapigwa Cairo, kwenye Uwanja wa Juni 30.