Aussems atimka akitoa masharti Simba

Muktasari:

Aussems ameenda mapumziko na anatarajiwa kurejea siku chache kabla ya timu kutimka kwenda kambini kwa maandalizi ya msimu mpya, lakini akitaka nafasi ya Kocha wa Makipa iboreshwe ili nafasi hiyo iwe na ushindani wa kweli katika kikosi chache kijacho.

KOCHA Patrick Aussems anayeinoa Simba, alfajiri ya juzi Jumamosi ametimka kwenda kwao Ubelgiji, huku akiacha masharti kwa Wakurugenzi wa Bodi ya klabu hiyo hasa kwa upande wa kikosi kipya na benchi la ufundi atakalofanya nao kazi msimu ujao.
Aussems ameenda mapumziko na anatarajiwa kurejea siku chache kabla ya timu kutimka kwenda kambini kwa maandalizi ya msimu mpya, lakini akitaka nafasi ya Kocha wa Makipa iboreshwe ili nafasi hiyo iwe na ushindani wa kweli katika kikosi chache kijacho.
Iko hivi. Aussems katika ripoti yake ya msimu mzima ameomba Kocha wa sasa wa Makipa, Mohammed Muharami ‘Shilton’ akaongezewe ujuzi, ila ikishindikana basi aletwe kocha mwingine ambaye ataboresha uwezo wa makipa wa timu hiyo Aishi Manula, Deo Munishi ‘Dida’ na Ally Salim kwa msimu ujao.
Mbali na hilo, lakini Mwanaspoti linafahamu Aussems pia ameomba mabosi wa Simba kumletea mtaalamu wa viungo (Physiotherapist), kutoka nje ya nchi anayefahamu aina tiba na misosi itakayopunguza majeruhi ndani ya kikosi chake.
Aussems aliliambia Mwanaspoti kuwa maboresho hayo yanayofanyika kuanzia benchi la ufundi na kuleta vifaa vipya yote ni kuhakikisha kikosi cha Simba kinakuwa imara zaidi ya msimu uliopita na kufikia yale malengo ya muda mfupi kwa maana ya kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara, kufika mbali kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.
“Ni kweli mtu wa Physiotherapy ili kupunguza majeruhi ndani ya timu kama ilivyokuwa msimu huu kwani wao ndiyo wana ufahamu mkubwa katika tiba, vyakula na mazoezi ili mchezaji aweze kupona kwa muda mfupi,” alisema Aussems.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohammed ‘MO’ Dewji na baadhi ya wajumbe wa bodi ya Wakurugenzi wamekutana kuifanyia kazi ripoti hiyo ya kocha Aussems katika kusajili nyota wa maana hasa maeneo yanayohitaji kuboreshwa.
Ripoti ya Aussems mbali ya kutaka wachezaji wapya wa maana wasiopungua wanne, pia amemuomba Mo Dewji wamuongezee mkataba wa mwaka mmoja Kocha Msaidizi Denis Kitambi aliyesaini makataba mfupi alipotua klabuni hapo.
Kitambi alisaini mkataba wa miezi minne, lakini Aussems kwa kuridhishwa na kazi yake ametaka apewe mkataba mrefu ili waijenge kwa pamoja Simba.
“Aussems alituambia wanafanya kazi vizuri na kwa maelewano makubwa, hivyo kutaka aongezwe mkataba,” alisema kigogo mmoja.