Mastaa wa Liverpool maisha yanataka nini tena

Muktasari:

Firmino alimwaga mvinyo kwenye vyumba vya kubadilishia na alipiga selfie na Wabrazili wenzake, Fabinho na Alisson, wakiwa na medali zao

LIVERPOOL, ENGLAND. KWA masupastaa wa Liverpool maisha yanahitaji nini tena zaidi ya kujimwaga tu na mademu zao kujipongeza baada ya kubeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Mastaa wa kikosi hicho cha Kocha Jurgen Klopp walitumia vyema kabisa fursa ya kushangilia ubingwa wa Ulaya kwa kufurahia na mademu zao huko Madrid baada ya kumalizika tu kwenye mechi ya fainali ambapo waliichapa Tottenham Hotspur 2-0, shukrani kwa mabao ya Mohamed Salah na Divock Origi.
Kuanzia kwa bosi mmiliki wa timu, John W Henry alifurahia ubingwa huo akiwa na mkewe, mrembo Linda Pizzuti, ambaye alikuwa amepigilia kivazi chekundu kuendana na jezi za wababe hao wa Anfield.
Hilo liliwafungulia mastaa wa timu hiyo na kuamua kufurahia na wanawake zao, akianzia Alex Oxlade-Chamberlain, aliyekuwa na mrembo wake, Perrie Edwards, wakati mshambuliaji Roberto Firmino naye alionekana akifurahia ubingwa huo na mkewe mrembo, Larissa Pereira kwenye Uwanja wa Wanda Metropolitano.
Alberto Moreno naye hakubaki nyuma akijiachia na mkewe, mrembo Lilia Granadilla.
Kipa Alisson hakupata muda wa kuwa na mkewe uwanjani hapo, lakini alimpigia simu ya video na kumwonyesha mkewe, mrembo Natalia Loewe Becker medali ya ubingwa aliyobeba na kufanya kuwa usiku wa Liverpool kutamba na mademu zao.
Baada ya kuondoka uwanjani na kuingia vyumbani, sherehe hiyo iliendelea usiku wote hata walipokuwa kwenye basi pia. Firmino alimwaga mvinyo kwenye vyumba vya kubadilishia na alipiga selfie na Wabrazili wenzake, Fabinho na Alisson, wakiwa na medali zao.