Migne atuliza presha kogalo

Muktasari:

Baada ya msimu kumalizika rasmi na Gor kukabidhiwa taji lao, Oktay ataondoka na kwenda kwao Uturuki kwa ajili ya likizo kisha atarejea baada ya dimba la AFCON kuanza maandalizi ya msimu mpya.

KOCHA wa Gor Mahia, Hassan Oktay kasisistiza hataitosa klabu hiyo baada ya kuiongoza kutwaa taji lake la tatu mfululizo la ubingwa wa Ligi Kuu nchini KPL.
Oktay aliyejiunga na Gor mapema msimu huu angali na mwaka mmoja kwenye mkataba wake, klabu kadhaa zimekuwa zikimuulizia.
Lakini akizungumza hivi majuzi baada ya kutuzwa tena kuwa kocha bora wa Mwezi Aprili, Oktay kasisitiza hana mpango wa kuigura Gor.
Oktay aliyetuzwa kocha bora Mwezi Februari vile vile, kafichua amekuwa kwenye majadiliano na Mwenyekiti wa Gor, Ambrose Rachier na wapo katika hatua nzuri ya kufikia makubaliano yatakayohakikisha anadumu klabuni.
“Klabu kadhaa kutoka Uturuki na Afrika zishanitokea zikihitaji huduma yangu ila nimeweka wazi kwamba bado nina mkataba na Gor. Naamini bado sijamaliza kazi yangu hapa hivyo nitaendelea kujadiliana na mwenyekiti kuhakikisha tunatatua baadhi ya mambo madogo kabla ya msimu ujao,” Oktay kasema.
Baada ya msimu kumalizika rasmi na Gor kukabidhiwa taji lao, Oktay ataondoka na kwenda kwao Uturuki kwa ajili ya likizo kisha atarejea baada ya dimba la AFCON kuanza maandalizi ya msimu mpya.
Gor walitwaa ubingwa wao wa 18 na tatu mfululizo juzi Jumatano zikiwa zimesalia mechi mbili, kufuatia sare ya kufungana bao 1-1 na Vihiga United , baada ya wapinzani wa karibu Bandari FC kutoka sare tasa na Mathare.
Kwa ujumla Gor wamezoa alama 70 na hata endapo watapoteza mechi mbili walizosalia nazo nao Bandari wenye alama 62 washinde zao zote, bado hawataweza kuwafikia.