Ubingwa Simba wapelekwa Morogoro, mashabiki Dar wanuna

Saturday May 25 2019

Mwanaspoti, Ubingwa, Simba, wapelekwa, Morogoro, mashabiki Dar wanuna

 

By OLIPA ASSA

Dar es Salaam. Kukosekana kwa mgeni rasmi Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola kumetajwa ndiyo sababu ya Simba kutokabidhiwa kombe la ubingwa wa Ligi Kuu Bara na sasa itafanyika hivyo Jumanne kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Leo Jumamosi, Simba walipaswa kukabidhiwa kombe katika mchezo wake wake dhidi ya Biashara United uliomalizika kwa sare 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa.

Wakati mechi hiyo iliyoshudiwa na mashabiki wachecha kwenye Uwanja wa Taifa ikiendelea klabu ya Simba ilitoa taarifa kuwa ubingwa usingekabidhiwa kutokana na mvua, lakini mwisho bodi ya ligi ilisema ni kutokana kutokuwepo kwa mgeni wa heshima.

Mkurungezi wa bodi ya Ligi, Boniface Wambura alisema walishindwa kukabidhi kombe hilo kutokana mgeni ramsi Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola kupata dharura.

Wambura alisema; "Kila kitu kitakamilika mjini Morogoro ambapo itakuwa ndiyo mechi ya mwisho ya Ligi Kuu, tumeshindwa kukabidhi kombe kwasababu mgeni ramsi hajafika, amepatwa na dharura. Tunaipongeza Simba kutwaa ubingwa, ligi ilikuwa ndefu kwasababu timu zipo nyingi.

"Tulikuwa na changamoto nyingi ikiwemo mabadiliko ya ratiba yaliyotokana na mechi za CAF pamoja na kukosa udhamini, hivyo msimu ujao tutajipanga kuona mambo yanakwenda vizuri," alisema Wambura

Advertisement

Mchambuzi Ally Mayai aliishauri bodi hiyo kufanya mawasiliano ya mapema na mgeni rasmi ili kuepusha mabadiliko yasiyokuwa na ulazima.

"Kuahirisha kupewa ubingwa kunapunguza zile shangwe za awali, kwani mawasiliano walitakiwa wayafanye mapema, kukabidhiwa ubingwa nyumbani inapendeza kuliko ugenini," alisema Mayai.

Mechi hiyo haikuwa na mvuto kutokana mashabiki waliohudhuria wachache sababu kubwa ni mvua inayoendelea jijini Dar es Salaam ilisababisha hata uwanja wa Taifa uliotumika kutokuwa mzuri kuchezea mechi hiyo.

Katika mchezo huo Biashara United ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 13 kupitia Innocent Edwin kabla ya Simba kusawazisha kupitia kiungo wake, Clatous Chama katika dakika ya 16.

Kwa matokeo hayo, Simba imefikisha pointi 92 wakati Biashara United wenyewe wakifikisha 44, sasa wanahitaji kushinda mechi yao ya nyumbani ili kujinasua katika janga la kushuka daraja.

Mashabiki wa Simba watibukwa

Mashabiki wa Simba walijitokeza uwanjani leo, wamejikuta wakiingiwa nyongo baada ya kubaini kombe halikabidhiwi.

Baada ya mechi ya timu hiyo kumalizika dhidi ya Biashara, mashabiki walikaa mkao wa kulisubiria kombe ajabu wakaona hakuna maandalizi yoyote yanayofanyika ndipo wakagundua jambo hilo halitafanyika.

Wapo walioamua kukomaa mpaka mwisho kuona nini kitajiri lakini mwisho wa siku waliishia kunung'unika.

Wapo waliokuwa wanalalamika kuwa hawajatendewa haki kwa madai kwamba hawana uwezo wa kusafiri sababu wakitaja kuwa ni kukosa pesa.

Hata hivyo hakukuwa na mtu wa kusikiliza malalamiko yao ama kuwajibia waliamua kukubali matokeo na kuondoka

Advertisement