Zahera kutangaza kikosi kipya mechi na Azam FC

Muktasari:

Kocha huyo pamoja na kuanza msimu vizuri, lakini amemaliza akiwa hajapata taji lolote huku Yanga ikimaliza Ligi Kuu ikiwa nafasi ya pili

Dar es Salaam. Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera amesema baada ya mchezo dhidi ya Azam FC atatangaza wachezaji atakaowasajili na wale watakaondoka katika klabu hiyo.

Zahera alisema tayari wameishafanya makubaliano na wachezaji saba wa kigeni na wawili wa ndani, lakini kila kitu ameahidi kukiweka wazi baada ya mchezo wao na Azam FC.

"Bado sijamaliza kazi, lakini niahidi tu kwamba baada ya kumalizika mechi na Azam FC kila kitu nitakiweka wazi ili kujua kikosi kipya ambacho nitafanya nacho kazi.

"Nitahitaji kupata wachezaji wenye ushindani wa hali ya juu kwa kuwa malengo ya msimu ujao ni makubwa, hivyo kikosi changu kitasheheni silaha za maana.

"Sina maana kwamba wale walikuwepo hawajafanya kazi hapana, ila kitu kina wakati wake na muda wake ukifika Watanzania ama mashabiki wa Yanga watakijua kikosi chao kipya," alisema Zahera.