Una pesa za mawazo? Pita kule, hapa pochi nene tu

Muktasari:

Neymar si mchezaji pekee ambaye ukitaka saini yake basi usiwe na pesa za mawazo, uwe na pochi nene na Kylian Mbappe anaongoza, kwamba ukimtaka hakikisha mfukoni una Euro 218.5 milioni.

LONDON, ENGLAND. LISEMWALO ni kwamba kwenye mkataba wa supastaa wa Kibrazili, Neymar kuna kipengele  kinachofichua unaweza kumsajili staa huyo kwa Euro 170 milioni tu itakapofika mwakani.
Lakini ukitaka kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi, basi bila ya shaka utatakiwa ujipange, uwe na pochi nene, pengine kuliko lile la Euro 222 milioni ambalo ililipa Paris Saint-Germain iliponyakua huduma yake kutoka Barcelona miaka miwili iliyopita.
Kuna wanaosema thamani halisi ya Neymar huko sokoni ukimtaka kwa sasa, basi jiandaye na mkwanja usiopungua Euro 197.1 milioni.
Hata hivyo, Neymar si mchezaji pekee ambaye ukitaka saini yake basi usiwe na pesa za mawazo, uwe na pochi nene na Kylian Mbappe anaongoza, kwamba ukimtaka hakikisha mfukoni una Euro 218.5 milioni.
Kuna timu kibao zinamtaka Mbappe, lakini ukweli saini yake si kila timu inayoweza kuimudu, huku wadau wa soka wakiamini staa huyo atauzwa kwa pesa itakayovunja rekodi ya Neymar ile ya Euro 222 milioni.
Straika Harry Kane naye yupo kwenye orodha, ambapo fowadi huyo wa Tottenham amedaiwa saini yake itakubidi ujiandae na Euro 200.3 milioni, huku Mohamed Salah wa Liverpool pia akidaiwa kupatikana kwa pesa ndefu, haipungui Euro 184.3 milioni, akizidiwa kidogo tu na Raheem Sterling, ambaye thamani yake imetajwa ni Euro 185.8 milioni kutokana na kiwango chake matata alichokionyesha huko Manchester City msimu huu.
Antoine Griezmann ameshaaga huko Atletico Madrid, lakini kitu kilichobaki ni timu za kumnunua tu, ambapo Barcelona inamtaka huku akidaiwa saini yake huwezi kuipata kwa mkwanja usiofikia Euro 155 milioni.
Paul Pogba anayehusishwa na Real Madrid ameripotiwa kwenye soko saini yake unaweza kuipata kwa Euro 130.3 milioni.  Vichwa vyote hivyo vinahitaji pesa ndefu kuvikamatia.
Staa wa Chelsea, Eden Hazard licha ya kubaliza mwaka mmoja kwenye mkataba wake huko Stamford Bridge, saini yake bado ghali, bila ya Euro 129 milioni huwezi kupata huduma yake, huku mchezaji Sadio Mane, naye akidaiwa kuwa juu, Liverpool haitakubali kumuuza kwa dau lisilofikia Euro 130 milioni.
Philippe Coutinho, Dele Alli, Bernardo Silva, Ousmane Dembele na hata Paul Dybala ni wachezaji wengine wanaotajwa kuwa saini zao bado zipo juu sana na ukitaka kuwanasa, basi usiende na mkwanja usiofikia Euro 100 milioni, labda kama wataamua kukuuzia tu.
Leroy Sane anayewindwa na Bayern Munich naye bei yake imechangamka, ambapo huko sokoni inadai staa huyo ana thamani ya Euro 150 milioni, licha ya Man City kudai Bayern ikiweka mezani Euro 102 milioni watafanya biashara.