Nandy: Eti Ruby! Mbona kiroho safi tu

Muktasari:

Awali, ilikuwa ikielezwa kuwa mastaa hawa wako kwenye bifu kali huku Nandy akisukwa kwa ajili ya kumpiku Ruby katika game

Dar es Salaam.NANI kasema kuna bifu kwenye mishemishe za kutafuta pesa a.k.a mkwanja! Sasa masuala ya bifu wakati wa kupiga dili za kuingiza mkwanja wa maana hayapo kabisa kwa masupastaa wa kike wanaosumbua kwa sasa kwenye Bongo Flava, Nandy na Ruby.

Awali, ilikuwa ikielezwa kuwa mastaa hawa wako kwenye bifu kali huku Nandy akisukwa kwa ajili ya kumpiku Ruby katika game, lakini kumbe aah wapi buana.

Sasa sikia hii. Nandy amefunguka kuwa yuko tayari kumshirikisha Ruby kwenye shoo yake ya Eid El-Fitri itakayofanyika katika Uwanja wa Mandela mjini Sumbawanga.

Nandy kwa sasa yuko anga za mbali kabisa kwenye game, alisema hana bifu kabisa na Ruby na kwamba, hizo ni hisia za watu tu.

Hata hivyo, alisema kuwa amekuwa akimsikia Ruby kwenye vyombo vya habari na watu wanaotajwa kumuunga mkono kwenye mitandao wakizoza, lakini kwake hana tatizo kabisa.

“Narudia tena jamani sina tatizo na Ruby na nipo tayari kama atakuwa tayari kupanda stejini kwenye shoo ya Sumbawanga. Nimesema mara kadhaa kwamba, sina bifu na mtu. Nimesikia watu wanasema eti hatuelewani…sijui huyu ni bora kuliko yule, kwangu mambo haya hayana nafasi na huwa nakuwa kimya siku zote,” alisema Nandy.