Biashara United yajinasua kutoka mkiani, Ruvu Shooting njia panda

Monday May 20 2019

Mwanaspoti, Michezo, Biashara United, yajinasua, mkiani, Ruvu Shooting, Michezo blog, Mwanasport

 

By Olipa Assa

Dar es Salaam. Biashara United imepanda kwa nafasi tatu kutoka mkiani baada ya kuichapa Ruvu Shooting kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Karume, Mara.

Ushindi huo umeifanya Biashara United kufikisha pointi 43 na kupanda kutoka nafasi ya 18 hadi 15, huku Ruvu Shooting ikishuka kutoka nafasi ya 16 mpaka 18.

Biashara United imejiweka katika nafasi nzuri ya kubaki katika Ligi Kuu iwapo itashinda mechi zake mbili zilizobaki wakati Ruvu Shooting imebakiwa na mechi moja mkononi baada ya kucheza mechi 37, na kuvuna pointi 42.

Katika mchezo huo wenyeji Biashara United ilitumia vizuri dakika 45 za kipindi cha kwanza, kupata mabao mawili kupitia kwa mshambuliaji wake Tariq Self Kiakala, dakika ya 29 na 42.

Kipindi cha pili Ruvu Shooting iliingia kwa kushambulia zaidi na kufanikiwa kupata bao lililofungwa na Fullzulu Maganga kwa mkwaju wa penalti baada ya beki ya Biashara kushika mpira katika eneo la penalti.

Kocha wa Biashara, Amri Said alisemaa mchezo huo ulikuwa muhimu kwao kupata pointi tatu za kuwaweka salama kwenye msimamo wa ligi ili kujilinda na kushuka daraja.

Advertisement

"Mchezo ulio mbele yetu ni dhidi ya Simba, tunajipanga kuhakikisha tunapata pointi tatu ambazo zitakuwa zinatuhakikishia kubaki kwenye ligi ya msimu ujao," alisema.

Kocha wa Ruvu Shooting, Abdulmutik Haji alisema hawana budi kuangalia mchezo wao wa mwisho baada ya kupoteza dhidi ya Biashara.

"Unajua mechi za mwisho zina presha kubwa, tumepoteza tunaelekeza akili kwetu vitu vya faida kwetu," alisema kocha Haji.

 

 

 

 

 

 

 

 

Advertisement