Mo Salah: Bado nne tu tubebe ubingwa wetu Liverpool

Muktasari:

Liverpool wamelinda pengo lao la pointi mbili kileleni licha ya kwamba wao wana mechi moja zaidi kuliko wapinzani wao Man City.

LIVERPOOL, ENGLAND. HUKO kwenye Ligi Kuu England kumenoga. Vita ya kusaka ubingwa inayopiganwa baina ya Liverpool na Manchester City imefikia patamu, kila mmoja akishinda mechi zake. Juzi Jumapili, Man City walianza kwa kuwachapa Crystal Palace wakidhani kwamba wenzao Liverpool watakwama kwa Chelsea huko Anfield, lakini chama hilo la Jurgen Klopp lilitoa kipigo cha 2-0 na supastaa Mohamed Salah, akasema bado mechi nne tu tuubebe ubingwa wetu.
Katika mechi hiyo, Mo Salah alikuwa miongoni mwa waliotikisa nyavu akipiga bao la pili baada ya lile la kwanza kufungwa na Msenegali, Sadio Mane na kuwafanya kurudi kieleleni kwenye msimamo wa ligi hiyo na pointi zao 85 baada ya kuenguliwa kwa muda na Man City. Liverpool wamelinda pengo lao la pointi mbili kileleni licha ya kwamba wao wana mechi moja zaidi kuliko wapinzani wao Man City.
Katika mbio za ubingwa, Mo Salah amewaambia wenzake wanahitaji kushinda mechi zao nne zilizobaki kujibebea ubingwa huo. Man City wao wamebakiza mechi ngumu dhidi ya Tottenham Hotspur na Manchester United na hapo ndipo anapoamini Mo Salah kwamba watakuwa na nafasi ya kujitanua zaidi mbele kama watazishinda Cardiff City, Huddersfield Town, Newcastle United na Wolves.
"Kwa maoni yangu ndio. Tunachopaswa kukifanya ni kutuliza tu akili zetu kwenyue mechi zote na tunaamini Manchester City watapoteza pointi," alisema Salah.
"Nimekuwa nikiwafuatilia Man City matokeo yao, yananipa matumaini, lakini nasi tunapaswa kucheza vyema. Tunahitaji kushinda, hatupaswi kupoteza pointi."
Liverpool kesho Jumatano watakipiga na FC Porto kwenye mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya robo fainali huku wakiwa na kumbukumbu ya kushinda 2-0 kwenye mchezo wa kwanza.