Nyota Cameroon arithi mikoba ya mama yake, Senegal, Morocco sare ya kwanza Afcon

Muktasari:

Mwaka jana (2018), Steve akiwa na miaka 16, aliibeba timu ya vijana ya Cameroon kutwaa ubingwa wa mashindano ya UNNIFAC kwa  kufunga mabao sita yaliyomfanya kuwa mfungaji bora.

Dar es Salaam. Amakweli mtoto wa nyoka ni nyoka,  hilo limejidhilisha kwenye mchezo wa kwanza wa kundi B katika fainali za mataifa ya Afrika chini ya umri wa  miaka 17  kwa  mtoto wa Marie Mvoue aitwaye Steven.

Steve ambaye ni mshambuliaji ameendeleza makali ya familia yake kwa kuitungua Guinea moja ya mabao muhimu yaliyoipa pointi tatu Cameroon kwenye mchezo wao wa kwanza uliochezwa uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.

Marie ni mwanamama wa Cameroon ambaye enzi zake alikuwa akicheza soka na aliwahi kuwa nahodha wa timu ya taifa hilo upande wa wanawake.

Katika mchezo huo wa kwanza kwa vijana wa Cameroon, walitangulizwa na mtoto wa mwanamama huyo, dakika ya 41 kabla ya kipindi cha pili kujipatia bao lao la pili.

Steve ameendeleza rekodi ya familia yake ambapo msimu uliopita kaka yake, Stephane katika fainali kama hizi nchini Gabon, 2017 aliifunga Guinea kwenye mchezo uliomalizika kwa sare ya bao 1-1.

Bao alilofunga Steve kwenye mchezo dhidi ya Guinea ni bao lake la 11 katika michezo 16 ambayo amekichezea kikosi cha Cameroon chini ya umri wa miaka 17.

Kinda huyo analelewa na mama yake kwenye akademi ya Azur Star huku upande wa kaka mtu, Stephane anacheza soka la kulipwa Ufaransa kwenye klabu ya Toulouse.

SENEGAL WAIVUTA SHATI MOROCCO

Vijana wa timu ya taifa la Senegal wameivuta shati Morocco kwa kulazisha sare ya bao 1-1 dakika za mwishoni mwa kipindi cha pili kwenye mchezo wa pili wa kundi B.

Morocco ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao kwenye mchezo huo ulioanza majira ya saa 11:00 jioni lililofungwa na Tawfik Bentayeb dakika ya 46.

Senegal walisawazisha bao hilo dakika ya 88 kupitia kwa Aliou Balde.