Kagere uso kwa uso na Kagere, atuliza mizuka ya mashabiki Simba

Muktasari:

Mtoto Shango ‘Kagere’ amejijengea umarufu katika mitandao ya kijamii kutokana na mapenzi yake kwa Simba hasa mshambuliali Meddie Kagere

Tanga/Dar. Rackim Shango ‘Kagere’ mtoto aliyejipatia umaarufu kwa kuishabikia Simba amesema alijisikia vibaya timu hiyo ilipofungwa mabao 4-1 na TP Mazembe na kuwataka mashabiki kusahau yaliyopita.

Akizungumza na Mwanaspoti online baada ya kutazama mazoezi ya Simba kwenye Uwanja wa Popatlal Jijini Tanga, Rackim alisema hakulala usingizi siku Simba ilipofungwa na TP Mazembe.

Mtoto huyo alisema soka ni mchezo wenye matokeo matatu kushinda, kufungwa na kutoa sare hivyo Simba itajipanga upya.

Akizungumzia mchezo wa Jumatano, Rackim amesema Simba itaifunga Coastal Union mabao matatu yatakayofungwa na Kagere na Okwi.

“Amewaomba mashabiki wa Simba kusahau yaliyopita na wajitokeze Uwanja wa Mkwakwani Jumatano kuishangilia Simba.”

Mshambuliaji Meddie Kagere amesema anajiona ni mwenye bahati ya ajabu kupendwa na watu wa lika zote na ndio sababu ya yeye kujituma kwa bidii.

Kagere amejizolea umarufu kutokana na staili zake za kushangilia ikiwemo kuziba jicho moja anapokuwa amefunga bao.

Kagere anasema anaheshimu mchango wa mashabiki ambao wanafuatilia kazi zake na amekuwa akijiona ni mchezaji mwenye bahati.

"Naheshimu sana mchango wa mashabiki wanaotoa kwa ajili yangu, napendwa na watu wote watoto na watu wazima hilo linanipa moyo wa kujituma kwa bidii.

"Nikitafakari ni watu wangapi ambao wanacheza, lakini hawajabahatika kupendwa, nawasbukuru na waendelee kuiunga mkono Simba ili tutetee ubingwa kwa pamoja" anasema.

Kagere amejizolea umarufu mwingine baada ya kushangilia kwa wimbo wa tetema Simba baada ya kuwafunga Yanga bao 1-0 mechi ya mzunguko wa pili.