Neville: Mata, Herrera, Pogba wakiondoka wala hajutii

Muktasari:

Wakati kocha Ole Gunnar Solskjaer akijiandaa kufanya usajili mkubwa mwishoni mwa msimu huu kwa kuwanasa mastaa kibao wanaotajwa kama Kalidou Koulibaly, Jadon Sancho na Aaron Wan-Bissaka kuna wachezaji wengine wataondoka

Manchester, England. Gwiji wa Manchester United, Garry Neville ametoa orodha ya wachezaji wanne akidai kwamba wakiondoka hakuna hata mtu mmoja atakayeteseka!
Wakati kocha Ole Gunnar Solskjaer akijiandaa kufanya usajili mkubwa mwishoni mwa msimu huu kwa kuwanasa mastaa kibao wanaotajwa kama Kalidou Koulibaly, Jadon Sancho na Aaron Wan-Bissaka kuna wachezaji wengine wataondoka kwenye timu hiyo ya Old Trafford, lakini Neville anadai kuna mastaa wanne wakiondoka, hakuna atakayekuwa amewamisi.
"Kuna wachezaji wengi Ole atahitaji kufanya uamuzi. Ni hasara Darmian akiondoka? Sidhani kama itakuwa mwisho wa dunia. Ni pigo Antonio Valencia akiondoka? Anasumbuliwa sana na majeruhi, nadhani United inahitaji beki mpya wa kulia. Ashley Young, ana nafuu na yupo kwa miezi mingine 12," alisema Neville.
"Nadhani Mata (Juan) na (Ander) Herrera wanawindwa na timu nyingine. Nadhani hao ni wachezaji wanaotakiwa na timu nyingine, kwangu mimi sioni kama itakuwa mwisho wa dunia kama wote wataondoka."
Wakati huo huo, wachezaji wa Man United wameripotiwa kwamba watakatwa mishahara yao kwa asilimia 25 kila mmoja kama timu hiyo itashindwa kukamatia nafasi kwenye Top Four ili kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Taarifa za kutoka Old Trafford zinafichua hivyo, huku kukiwa na madai kwamba mambo kama hayo ndiyo yatakayomfanya supastaa Paul Pogba kukusanya virago vyake na kuondoka kuliko kubaki kwenye timu hiyo akatwe mshahara na timu ikiwa imekosa kufuzu kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao.