Serengeti Boys yaichapa Cameroon mabao 2-1, Kelvin ‘Mbappe’ aumia akimbizwa hospitali

Muktasari:
Serengeti Boys inajiandaa na mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa vijana U17 yatakayofanyika Dar es Salaam Aprili 14-28, 2019
Dar es Salaam. Mshambuliaji wa tegemeo wa Serengeti Boys, Kelvin John aumia na kupelekwa hospitali wakati wa Tanzania ikichapa Cameroon kwa mabao 2-1 katika mchezo wa kirafiki uliochezwa kwenye Uwanja wa Nyamirambo, Rwanda.
Serengeti Boys ilipata mabao yake mawili kupitia Abraham Morice dakika 8, na Swakali Arafat (92) huku bao la kufutia machozi la Cameroon likifungwa na Yannick Noah.
Ushindi huo wa Serengeti Boys umepata pigo baada ya mshambuliaji wake Kelvin ‘Mbappe’ kuumia katika kipindi cha kwanza baada ya kugongana na mchezaji wa Cameroon alipatiwa huduma ya kwanza uwanjani hapo kabla kupelekwa hospitali kwa matibabu zaidi.
Kuumia kwa Kelvin ni pigo kwa Serengeti Boys inayojiandaa na mashindano ya Afcon yatakayofanyika Dar es Salaam kuanzia Aprili 14-28, 2019.
Serengeti Boys ipo Rwanda ambako inacheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Rwanda na Cameroon ikiwa ni sehemu ya maandalizi yake ya fainali za Afcon.
Katika mchezo dhidi ya Cameroon, Serengeti Boys ilianza vizuri na kufanikiwa kupata bao la kuongoza dakika 9, lililofungwa na Abraham Morice lililodumu hadi mapumziko.
Mwanzoni mwa kipindi cha pili Cameroon ilisawazisha bao hilo dakika 58, kupitia Yannick Noah baada ya mabeki wa Serengeti Boys kushindwa kuokoa hatari golini.
Hata hivyo, jobo la madaktari wa Serengeti Boy linabidi kufanya kazi ya ziada kuhusu hali ya wachezaji wake baada ya wengi kuumia na kupatwa na matatizo ya kushikwa na misuri.
Serengeti Boys ilipata bao la pili katika dakika 92, kwa mpira wa adhabu uliopigwa na Arafat na kwenda moja kwa moja wavuni na kuamsha shangwe kwa benchi la Tanzania.