Kipa wa Zahera agomea mkataba

Yanga inataka kuboresha eneo lake la makipa kutafuta kipa wa maana na hesabu zao bado zipo kwa kipa wa Bandari ya Kenya, Farouk Shikalo na sasa habari mpya ni kugomea mkataba mpya na klabu yake.

Bosi mmoja wa Yanga ameliambia Mwanaspoti kuwa baada ya usajili wa kipa huyo kukwama dirisha dogo bado wanahitaji huduma za mlinda mlango huyo wa kikosi cha Bandari ya Kenya ambaye wamemtaka kutoongeza mkataba katika klabu yake.

Aliongeza kuwa lengo lao kutoingia katika ugumu wa kumnasa kipa huyo ili wamnase kipa huyo ambaye mkataba wake unafikia tamati Desemba mwaka huu katika kikosi chake cha Bandari.

Shikalo, ambaye msimu uliopita alikuwa kipa bora wa Ligi Kuu Kenya alikubalika kwa kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera na kumfanya awe mbogo bada ya kusikia usajili wake umekwama.

Shikalo kwasasa ndiye mchezaji pekee aliyeitwa katika kikosi cha Kenya ‘Harambee Stars’ akiwa kipa namba mbili huku kocha wa timu hiyo Mfaransa Sébastien Migné.

“Bado tuna akili ya kuchukua kipa na bado tunafanya mawasiliano na Farouk unajua usajili wake wakati ule ulikwama kutokana na upungufu wa fedha klabu yake ilihitaji fedha nyingi.

“Tumemwambia kwamba asiongeze mkataba asubiri hadi Mei mwaka huu tuangalie kipi tutakubaliana na klabu yake, unajua akiongeza bei yake itakuwa juu zaidi na kama akifanya hivyo inamaana tutaachana naye na tuangalie kipa mwingine.”