Kigogo Yanga kakubali yaishe kwa Zahera

Muktasari:

Sauko kafunguka kuwa, kwa sasa Simba wanaogelea kwenye utajiri wa Mohamed Dewji (MO), lakini Yanga imeendelea kula nao sahani moja kwa sababu kwenye benchi la ufundi kuna Zahera.

Dar es Salaam. Yanga wana hali mbaya kifedha, lakini uwanjani wanaendelea kutimua vumbi na kukaa kileleni mwa msimamo kwa muda mrefu. Lakini, misimamo na ubunifu wa kocha wao, Mkongomani Mwinyi Zahera ndio imetajwa kuwa mpango mzima.

Si unamkumbuka aliyekuwa Katibu Mipango wa Yanga, Abdul Sauko, ndio huyo huyo sasa jamaa kafunguka kuwa kama sio Zahera basi mambo yangekuwa mabaya kwelikweli kwa Wanajangwani hao na suala la furaha lingekuwa stori tu.

Sauko kafunguka kuwa, kwa sasa Simba wanaogelea kwenye utajiri wa Mohamed Dewji (MO), lakini Yanga imeendelea kula nao sahani moja kwa sababu kwenye benchi la ufundi kuna Zahera.

Sauko amesema sio jambo rahisi hata kidogo kwa kocha mwenye viwango vya kimataifa kama Zahera, kuvumilia hali ya ukata kisha akawajenga wachezaji wake kupambana kwa hali na mali kwa ajili ya timu na wakafanikiwa kuongoza ligi mpaka sasa.

Alivichambua vitu adimu alivyoviona kwa Zahera akitaja kuwa, hana uoga wa kuzungumza ukweli na kukemea jambo ambalo haliendi sawa iwe kwa viongozi ama wachezaji kitu ambacho kimekuwa kikibeba Yanga Yanga na kuifanya kusimama imara kama timu.

"Kama Zahera angekosa msimamo ingekuwa ngumu kwa Yanga kuendelea kuwepo kwenye mstari wake…kuna mambo mengi yanaendelea kwa sasa ikiwemo uchaguzi na ukata, lakini Zahera amesimamia kile anachokiamini katika taaluma yake na hajakubali kuyumbishwa.

"Zahera ni mbunifu ndio maana amefungua akaunti ya benki kwa ajili ya wanachama kuchangia timu, yote ni kuhakikisha mambo yanakwenda sawa," alisema.

Jambo lingine aliloliona Sauko kwa Zahera alilitaja kuwa hajatengeneza makundi kwenye timu na kudai amewafanya wachezaji wote kuwa sawa na kujenga nidhamu na umoja.

"Hakuna kitu kizuri kama wachezaji kujengwa akili kuwa, wapo sawa na wote ni muhimu kwa klabu…hakuna mtu muhimu kuzidi wengine," alisema.

Kwa upande wake Zahera alisema, anaamini katika kusimamia taluma yake na kuwaambia ukweli wachezaji ili wafahamu ni kitu gani kinatakiwa kwenye soka.

"Soka ni mchezo wa wazi, hakuna mambo ya kupindisha pindisha, mfano mchezaji anapaswa kuwa na nidhamu ya kuutunza mwili wake kwa ajili ya kazi… nikimanisha mazoezi, uchezaji wake na kulinda kiwango.

"Ndio maana kwangu hata mchezaji akipata kadi ataendelea na mazoezi kama kawaida…hakuna likizo anatakiwa kufanya mazoezi kwa bidii ili kujiweka kwenye mipango ya kocha," alisema.

Mbali na hilo alizungumzia maandalizi kuelekea mchezo wao na KMC kwamba, wanaendelea na mazoezi na wanawaheshimu wapinzani wao ila kikubwa kwake ni kupata pointi tatu.