Kesi ya Aveva, Kaburu wakwama

Muktasari:

Katika shtaka lingine inadaiwa Aveva, Nyange na Hans Poppe kati ya March10 na September 30, 2016 waliwasilisha nyaraka za uongo kuonyesha Simba imenunua nyasi bandia zenye thamani ya Dola za Kimarekani 40,577.

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jana Ijumaa imeshindwa kuendelea na ushahidi katika kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili vigogo wa klabu ya Simba kutokana na mawakili wa upande wa utetezi kuwa na kesi nyingine Mahakama Kuu.
Vigogo hao ni Rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva, Makamu wake, Geofrey Nyange 'Kaburu na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa klabu hiyo, Zacharia Hans Poppe.
Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Leonard Swai jana alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba  kuwa Kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa licha ya Shahidi kuwa na tatizo la kiafya lakini mawakili wa utetezi wapo Mahakama Kuu.
"Upande wa utetezi tulimwandaa shahidi ambaye ni meneja wa benki ya Baclays lakini amepata tatizo la kiafya pamoja na hayo mawakili wa utetezi wako Mahakama kuu tunaomba tarehe nyingine" alidai Wakili Swai
Mshtakiwa wa kwanza Evans Aveva alidai anatakiwa kubadilishwa figo ambapo itamchukua muda mrefu kulazwa hospital hivyo kuiomba Mahakama ijitaidi kumaliza kesi hiyo mapema.
Hata hivyo baada ya maelezo hayo Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 11 na 16  mwaka huu nakuutaka upande wa mashtaka kuhakikisha wanaleta mashahidi ili kesi hiyo iweze kukamilika kwa wakati.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 10 ikiwemo kula njama, kughushi, kuwasilisha nyaraka za kughushi,  kutoa maelezo ya uongo na utakatishaji wa fedha.
Katika shitaka la utakatishaji fedha linalomkabili Aveva, inadaiwa Machi 15, 2016 katika benki ya Baclays Mikocheni, Dar es Salaam alijipatia Dola za Kimarekani 187,817, takriban Sh. Milioni 400 kutoka katika Timu ya Simba wakati akijua zimetokana na zao la kosa la kughushi.
Katika shitaka la kughushi linawakabili washtakiwa wote, ambapo wanadaiwa katika tarehe hizo hizo kwa pamoja walighushi hati ya malipo ya kibiashara ya Mei 28, 2016 wakionyesha kwamba nyasi bandia zilizonunuliwa na Simba zinathamani ya dola 40,577 sawa na zaidi ya Sh. Milioni 90 huku wakijua kwamba sio kweli.
Pia katika shtaka lingine inadaiwa Aveva, Nyange na Hans Poppe kati ya March10 na September 30, 2016 waliwasilisha nyaraka za uongo kuonyesha Simba imenunua nyasi bandia zenye thamani ya Dola za Kimarekani 40,577.