Pluijm: Azam ni upepo mbaya tu unapita

Muktasari:

Azam hadi sasa ipo nafasi ya pili katika msimamo wa ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 49 baada ya kucheza michezo 23, kushinda 14, kutoka sare mara saba na kufungwa michezo miwili.

Dar es Salaam.Kocha Mkuu wa Azam FC, Hans Van Pluijm amesema kikosi chake hakina tatizo lolote linalowafanya washindwe kupata matokeo katika michezo mitatu mfululizo na kuweka wazi ni upepo mbaya tu umewapitia.
Azam FC, imeanza kupata sare katika uwanja wake wa nyumbani dhidi ya Biashara, wakaenda Morogoro wakakubali kipigo cha bao 2-0, Iringa na Lipuli wakakubali sare ya bao 1-1 na Mbeya wamekubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons.
Pluijm alisema hakuna mchezo kati ya hiyo minne walijiandaa kwaajili ya kushindwa mipango yao ilikuwa ni kupata ushindi lakini mbinu ndani ya uwanja ndio zilizokuwa zinavuruga mipango yake.
"Hakuna timu ambayo inajiandaa kwaajili ya kufungwa kila timu zinamipango ya kushinda hivyo naweza kusema matokeo tunayoyapitia Azam sasa ni upepo mbaya upo upande wetu timu haina tatizo lolote naamini kuwa tumezidiwa mbinu na timu tulizokutana nazo na ndio maana tumepata matokeo hayo,"

"Tumeshafahamu tunakosea wapi tumerudi kujipanga upya ili kuondoa makosa madogo madogo yaliyotughalimu na kusababisha tunapata pointi mbili katika michezo minne mfululizo tuliyocheza japo ni moja ya matokeo katika mpira wa miguu," alisema.
Katika hatua nyingine alizungumzia ubora wa kikosi chake kuwa uwezo wa wao kufanya vizuri wanao na mipango yao ya kuhakikisha wanatwaa ubingwa wa Ligi haijafutika pamoja na kupoteza pointi nyingi hivi karibuni.
Alisema timu yake inacheza mpira na inatengeneza nafasi za kufunga lakini inakosa umakini ikipata nafasi hilo ameliona na anatarajia kulifanyia kazi kabla ya michezo mingine ili kupunguza gepu la pointi na timu ambayo wanakimbizana nayo.