Mreno aliyemng’oa Kichuya huyu hapa

Monday February 11 2019

 

By Eliya Solomon

Dar es Salaam.Shiza Kichuya, aliyekuwa winga hodari wa Simba aliyeitesa sana Yanga, ametua Pharco ya Misri anakokwenda kucheza soka ya kulipwa kwa mara ya kwanza nje ya nchi.

Mwanasoka nyota wa zamani wa Ureno, Jose Rui Lopes Aguas, ndiye aliyemvuta Kichuya katika klabu hiyo, baada ya kuvutiwa na kiwango chake alichokiona kupitia mkanda wa video.

Mreno huyo alipendekeza jina la mshambuliaji huyo mfupi, baada ya kucheza kwa kiwango bora katika mechi za Simba kwenye mashindano mbalimbali.

Aguas aliyezaliwa Aprili 28, 1960 alitumia saa kadhaa kuangalia mkanda wa winga huyo na baada ya kumaliza kuangalia alitoa jibu moja tu la kumtaka Kichuya katika kikosi chake.

Kocha huyo wa zamani wa timu ya Taifa la Cape Verde, anajua vyema soka la Afrika, hivyo haikuwa ajabu kupendekeza jina la Kichuya.

Aguas aliyewahi kuwika na klabu za Benfica na FC Porto akiwa mshambuliaji, amecheza michezo 291, amefunga mabao 120 katika misimu 12 ya Ligi Kuu Ureno.

Pia alikuwemo katika kikosi cha Ureno kilichoshiriki Fainali za Kombe la Dunia mwaka 1986 nchini Mexico ambako Argentina ilitwaa ubingwa.

Aguas anaweza kumtengeneza Kichuya kuwa tishio kwa kufunga mabao kutokana na enzi zake kuwa moto wa kuotea mbali. Kocha huyo aliwahi kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Hispania msimu wa 1990–1991.

Pia nguli huyo aliwahi kuwa mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, wakati huo Kombe la Ulaya msimu  1987–88, Aguas anakumbukwa kwa kutwaa tuzo ya mfungaji bora wa Kombe la FA mwaka 1985–1986.

Bila shaka Aguas anaweza kuwa sehemu ya mafanikio ya Kichuya endapo mchezaji huyo atazingatia nidhamu ndani na nje ya uwanja.

Mshambuliaji huyo alijiunga na Simba katika msimu wa mwaka 2016 akitokea Mtibwa Sugar ya Turiani, Morogoro. Haikuwa kazi rahisi Simba kupata saini yake kwani Yanga pia ilihusishwa na mpango wa kutaka saini yake kabla ya kutua Msimbazi.

Baada ya kuwika Mtibwa Sugar, Kichuya alipeleka makali Simba ambako alicheza kwa kiwango bora, lakini ujio wa kocha mpya Mbelgiji Patrick Aussems.

Shiza aliyekuwa akitesa kwa chenga za maudhi, mashuti makali ya mbali na kasi uwanjani chini ya kocha Mfaransa Pierre Lechantre, alipoteza dira mbele ya Aussems.

Kwa kuthibitisha hilo, mshambuliaji huyo anayetokea pembeni, amecheza idadi ndogo ya mechi katika mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kichuya, sasa anakwenda Misri kufufua kipaji chake akiwa Pharco inayoshiriki Ligi Kuu Misri.

Kichuya anaongeza idadi ya wachezaji wazawa wanaokwenda kucheza soka ya kulipwa nje ya nchi akiungana na mshambuliaji waw Mbeya City, Eliud Ambokile aliyejiunga na Black Leopards ya Afrika Kusini hivi karibuni.

Hata hivyo, Kichuya anakwenda Misri akiwa na kibarua kigumu cha kuinusuru

Pharco ambayo imemtoa kwa mkopo kwenda klabu ya ENPPI ya Cairo  inayomilikiwa na kampuni petroli  ya  Misri inayoitwa ENPPI  na hata jina lao la utani inaitwa ‘The Petroleum Club’.

Mara kadhaa wauza petroli hao ambayo timu yao ilianzishwa miaka 33 iliyopita, imepata nafasi ya kushiriki michuano mikubwa ya Afrika ngazi ya klabu.

Kazi kubwa ya Kichuya ni kuisaidia ENPPI SC  kujiondoa katika hatari ya kushuka daraja maana ipo nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Misri yenye timu 18 ikiwa ni tofauti ya pointi moja na El Daklyeh inayoshika nafasi ya 15.

Timu zinazoshika nafasi ya 16 na 17 katika mashindano hayo ni Wadi Degla na Al Ittihad.

Pharco

Pharco ilianzishwa miaka tisa iliyopita kwenye mji wa Alexandria, Misri. Pharco  ipo chini ya Mwenyekiti Ezz Bashar Helmy ambaye amekuwa na mikakati kadhaa ya kuhakikisha ndani ya kipindi kifupi wanashiriki Ligi Kuu.

Timu hiyo inatumia uwanja wa El Geish wenye uwezo wa kuingiza watazamaji 86,000  katika michezo yao ya nyumbani kwenye Ligi Daraja la Pili.

Pharco inanolewa na Jose Aguas ambaye enzi zake aliwahi kushinda mataji manne ya Ligi Kuu Misri, matatu akiwa na Benfica kwenye msimu 1986–87, 1990–91, 1993–94 na moja akiwa na FC Porto msimu wa 1989–90.

 

Advertisement