Rekodi ya Simba Dar mwarabu lazima akae

Monday February 11 2019

 

By Thobias Sebastian

Dar es Salaam.Hakuna neno sahihi la kuweka hapa zaidi ya kusema Mwarabu lazima akae. Timu zote zinazocheza Ligi ya Mabingwa Afrika, hakuna iliyokosea kwenye uwanja wake wa nyumbani.

Wachezaji 11 na mmoja wa mashabiki watakuwa 12, haitakuwa vingine vyovyote zaidi ya Simba kumkalisha kwenye Uwanja wa Taifa. Wawakilishi hao wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa watakuwa na kibarua kigumu kesho Jumanne katika mechi ya marudiano dhidi ya Al Ahly.

Miamba hiyo ya Ligi Kuu Bara inaingia kwenye mchezo huo wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza kwa mabao 5-0 katika mechi ya kwanza.

Simba wapo katika kundi ‘D’ na timu za Al Ahly ambao ndio vinara wa kundi hilo wakiwa na pointi saba, AS Vita wapo nafasi ya pili wakiwa na pointi nne, Simba pointi tatu na JS Saoura ndio wanaburuza mkia wakiwa na pointi mbili.

Ili Simba wapate nafasi ya kufuzu robo fainali, lazima wahakikishe wanapata ushindi katika mechi na Al Ahly ambao nao kama watashinda mechi hiyo watakuwa tayari wameshafuzu katika hatua inayofata.

Makala haya inakuletea mambo ambayo Simba wanatakiwa kuyafanya ili kuhakikisha wanashinda katika uwanja wa nyumbani kama malengo yao yalivyo ya kupata pointi tisa katika mechi tatu ambazo zote watacheza Taifa.

SAFU YA ULINZI

Simba katika mechi tatu ambazo wamecheza kwenye Ligi ya Mabingwa moja wakiwa nyumbani walipata ushindi dhidi ya JS Soura, lakini mbili dhidi ya AS Vita na Al Ahly zote walipoteza tena kwa kufungwa mabao matano katika kila mechi.

Katika mechi hizo ambazo walipoteza, moja ya sababu iliyochangia ni kuwa na safu mbovu ya ulinzi ambayo inashindwa kukaba hadi mwisho na kuzalisha makosa mengi ambayo yaliwaghalimu kwa kufungwa idadi hiyo ya mabao mengi katika mechi mbili.

Mabeki wa Simba walishindwa kabisa kukaba vizuri na kupitika kwa urahisi, lakini walionesha udhaifu mkubwa wa kutokuruka mipira ya vichwa pengine yalitokea haya yote baada ya kukosekana Erasto Nyoni ambaye ni majeruhi, lakini kwa soka ambalo walionyesha AS Vita au  Al Ahly hata kama angekuwepo labda ingepungua idadi ya mabao lakini kufungwa kulikuwa pale pale.

Ili Simba waweze kushinda katika mechi mbili ambazo zimebaki ambazo watacheza katika uwanja wao wa nyumbani lazima wahakikisha walinzi wao wote ambao watacheza mechi hizo lazima wapunguze au kutokufanya makosa kama hayo ambayo hugharimu timu kwa kiasi kikubwa. Wanatakiwa kusimama na mtu ile wanayouiita ‘Chama na Mogella’ kwamba mkali wao kila anapokwenda, kuna mtu wa kumtibulia. Kila mmoja akisimama na mtu wake, hawataweza kwenda.

Kingine ni kuwazubaisha kuotea. Wachezaji wa Simba walizubaishwa kama wanatengeneza offside kumbe kuna mtu anapasiwa na wenyewe wanabakia kushangaa, ndiyo staili wanayotumia Waarabu na hata ilifanya hivyo AS Vita na kuja kushtuka wameshafungwa.

UKABAJI TIMU NZIMA

Safu ya ulinzi ya Simba mbali ya kuonekana kuwa na upungufu wa kutokukaba mpaka mwisho na kushindwa kuokoa mipira ya vichwa lakini wachezaji wa timu nzima wamekuwa na shida katika kukaba na mara nyingi ukaba kwa macho.

Wachezaji wa Simba wengi wanaonekana ni mahiri pindi timu inapokuwa na mpira lakini wanapokuwa wakishambuliwa wao wengi wao wanashindwa kuwa bora katika kukaba jambo ambalo linawapa uhuru wachezaji wa timu pinzani kushambulia kwa urahisi.

Hatua hii ni kubwa katika Ligi ya Mabingwa kwa maana hiyo mechi zake zitakuwa ngumu na ushindani mkubwa kwa maana hiyo ili kuweza kuwamudu wapinzani vizuri wachezaji wa Simba wanatakiwa wote kuwa wanakaba vizuri kuanzia washambuliaji mpaka mabeki.

NAFASI ZA KUFUNGA

Dakika 90, za mechi na Al Ahly, Simba walikuwa wamezidiwa kila kitu lakini katika hatua hii wamekuwa wakifanya mambo mawili mechi ugenini huwa wanatengeneza nafasi chache za kufunga ambazo hushindwa kuzitumia.

Katika mechi za nyumbani kama hii ambayo watacheza kesho huwa wanatengeneza nafasi nyingi za kufunga na hutumia chache ambazo mara baada ya kuona wanaongoza kwa mabao 2-3, wachezaji wa timu hiyo huanza kucheza kawaida kana kwamba wameshamaliza kazi.

Ili Simba isonge mbele lazima icheze kwa umakini mkubwa na kutumia nafasi nyingi za kufunga na si kukosa nyingi kama alivyofanya John Bocco katika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mwadui, kwani wakishindwa kufanya hivyo wao Al Ahly ni timu kubwa ambayo inaweza kufanya lolote na ikapindua matokeo katika mchezo huo.

HALI YA HEWA

Katika mechi ya kwanza Simba dhidi ya Al Ahly muda wa mechi ulibidi kuwa ni saa 1:00 usiku, lakini wenyeji waliamua kubadilisha muda na kupeleka saa 3:00 usiku ambapo hali ya hewa ya nchini Misri huongezeka baridi linakuwa kali sana.

Hueanda miongoni mwa sababu ambazo zilichangia Simba kufungwa mabao mengi katika mechi hiyo ni kutokuzoea mazingira ya hali ya hewa ambayo ipo nchini humu labda wachezaji wengi walikuwa hawajazoea.

Katika mechi ya hapo nyumbani Simba nao wanauwezo wa kuweka mechi hata saa 8:00 mchana ili kupata faida ya hali ya hewa ya joto na mazingira yatakavyokuwa kwani muda huo hapa Dar es Salaam jua linakuwa kali sana labda kuwe na mawingi na mvua.

Msimu uliopita Simba katika Kombe la Shirikisho Afrika walitoka suluhu ya kufungana mabao 2-2 na Al Masry katika uwanja wa Taifa huku wakionekana kucheza soka safi na muda mwingi kutawala mpira na labda kama wangecheza muda wa mchana walikuwa na uwezo wa kupata matokeo ya ushindi.

MASHABIKI KUFURIKA

Katika mechi ya kufuzu hatua ya makundi Simba dhidi ya Mbabane Swallows ambapo walishinda mabao 3-1 katika uwanja wa Taifa moja ya sababu ambayo ilichangia kupata ushindi ni wingi wa mashabiki ambao walijitokeza katika mechi hiyo.

Mashabiki wa Simba walikuwa wengi ambao muda mwingi walionekana kushangilia mbali ya timu yao kuanza kufungwa bao la kuongoza, ili timu hiyo ifanye vizuri tena katika mechi hii ya nyumbani, wingi wa mashabiki wa timu hiyo utanatakiwa kuongezeka.

Simba imeweka kiingilio cha chini kuwa Sh2000.

Mashabiki wa Simba wanatakiwa kuwa na hamasa ya kutosha kujitokeza uwanjani kwa wingi ili kuishangilia timu yao muda mwingi wachezaji watapata hamasa ya kupambana na kuona jinsi gani wanaweza kupata ushindi, lakini hata kama matokeo yatakuwa tofauti na hivyo waendelee kushangilia na kukubaliana na hali halisi na si kuanza kuzomea.

Al Ahly katika mechi yao na Simba mashabiki wao walijitokeza kwa wingi na muda wote walionekana wakipiga shangwe la kuwashangilia muda wote.

MECHI YA YANGA

Simba mara baada ya kucheza mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly, mchezo unaofata katika Ligi Kuu Bara ni dhidi ya watani zao Yanga ambao wao watakuwa wametoka kucheza na JKT Tanzania.

Wachezaji,benchi la ufundi,  viongozi, mashabiki wa Simba wote wanatakiwa kuwekeza nguvu katika mechi na Al Ahly kwanza na kuachana na inayofata dhidi ya Yanga.

Kama watakuwa wanacheza huku akili yao ikiwa inafikilia mechi inayokuja dhidi ya watani zao Yanga watajikuta wanmafanya vibaya na kufanya makosa mengi ambayo yatachangia wao kupoteza mchezo huo.

Kama watawekeza nguvu ya kutosha katika mchezio huo kama walivyofanya dhidi ya JS Saoura wanaweza wakapa ushindi na pointi tatu wakafanikiwa kupata.

WASIKIE HAWA

Kocha wa zamani wa Yanga Kenny Mwaisabula alisema makosa makubwa ambayo aliyaona katika kikosi cha Simba kwenye iliyopita kwanza walizidiwa katika maeneo yote lakini hawakuwa wazuri katika kukaba timu nzima na kuwapa wapinzani mianya ya kufanya kila wanalotaka.

“Mechi ya hapa nyumbani kwanza wanatakiwa kuwa mahiri na fiti katika kukaba haswa katika safu ya ulinzi ambayo ilionekana kufanya makosa mengi, na kama wakiweza kukaba vizuri wananafasi ya kupata ushindi lakini ikiwa tofauti na hapo wasitegee matokeo ya aina hiyo,” alisema Mwaisabula.

Kocha na mchambuzi wa soka nchini Joseph Kanakamfumo anasema sababu za Simba kufungwa kwanza wakubali tu juu ya uwezo wa mchezaji mmoja mmoja upo juu kwa kuliko wa Al Ahly ukilinganisha na hawa wa kwetu.

“Simba walifungwa mabao mengi pamoja na kuwaheshimu wapinzani kwa maneno tu nje ya uwanja , ndani walishindwa kuwaheshimu, makosa ya Pascal Wawa yalifanya kupatikana kwa goli la tatu , aliamua kupanda na kwenda mbele bila sababu ambapo alipoteza mpira huko ambao ulizaa bao,” anasema.

Advertisement