Fid Q atoboa siri Bongoflavor kuchemka Tamasha la Sauti Busara

Sunday February 10 2019

 

By Rhobi Chacha

Zanzibar. Mwanamuziki Fareed Kubanda ‘Fid Q’ amesema sababu ya wanamuziki wengi wa Bongoflavor kushindwa kualikwa katika Tamasha la Sauti za Busara ni mazoea ya kuimba kwa playback jukwaani.

Fid Q alisema kinachowafanya wasanii wa muziki wa kizazi kipya kutohudhuria tamasha hili kama wanavyofanya wanamuziki wanaoimba singeli, ngoma za asili na Rege, ni kutokuwa tayari kujifunza.

"Tatizo baadhi ya wanamuziki wa muziki wa kizazi kipya huwa hawataki kujifunza mfano mimi nimewahi kutumbuiza katika tamasha hili, ninajua.

“Huku hakuna ubabaishaji, msanii unatakiwa uimbe kwa sauti yako jukwaani, walio wengi hili hawaliwezi. Idadi kubwa ya wasanii wamezoea kuimba kwa ‘playback’, (kuweka cd), ndiyo maana hata waandaaji wanashindwa kuwaalika, muziki tunaofanya sisi ni ule wa wenzetu, lakini tunashindwa kuuwakilisha ipasavyo, tumezoea kuimba kwa ‘playback’." alisema Fid Q

Fid Q alisema mwaka huu ni mara ya sita kushiriki tamasha hilo na kadri siku zinavyozidi kwenda, anajifunza vitu vingi kupitia nchi mbalimbali zinazokutanishwa na Tamasha hilo.

Advertisement