Cheki dogo wa Serengeti Boys anavyopita njia za Samatta

Muktasari:

Kocha wake hakuamini alichokiona kwa kiungo huyo na kuamua kuanza kumtania kwa kumwita jina la kiungo wa kifaransa, Ngolo Kante.

Dar es Salaam.UNAYAJUA maisha ya wakimbizi yalivyo? Achana na vile ambavyo kula yao ni kwa shida pamoja na kutokuwa na furaha juu ya maisha hayo yaani wao kambi popote.

Sasa unaambiwa nyota wa Ngorongoro Heroes aliyejipatia ujiko kupitia fainali za Afcon U17- 2017 akiwa na Serengeti Boys, Ally Ng’anzi naye soka lake ni kambi popote. wakati akianza kulisakata  soka kambi ilikuwapopote.

Unaweza kustuka kuwa kivipi kwake kambi ilikuwapopote, jamaa ni mzaliwa wa mkoani Mwanza na alizaliwa Septemba 3, 2000 mkoani mwanza ni mototo wa mwisho kwenye familia ya mzee Hamis na Bi. Mwajuma wenye watoto wanne.

Ally ambaye kiasili ni mtu wa Tanga, alipoanza kupata ufahamu aliandikishwa Buzuruga Shule ya Msingi ndipo maisha ya kambipopote yalipoanza kama mkimbizi vile yote hiyo ilisababishwa na kipaji chake cha soka.

Unajua ilikuwaje na alianzia wapi hadi kupata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha Serengeti Boys wale ambao walikuwa Gabon kwenye Afcon, 2017, songa nayo maana Ally alitembelea ofisi zetu za Mwananchi zilizopo tabata jijini Dar es Salaam.

Akiwa ofisini kwetu alifunguka mambo kibao yanayohusu safari yake ya soka kiujumla hadi alivyopata shavu la kucheza soka la kulipwa kwenye taifa la Jamhuri ya Czech ambalo ni la kipa wa zamani wa Chelsea, Petr Čech ambaye kwa sasa anaidakia Arsenal.

Sasa usipime hivyo vituko huko Ulaya alivyokutana navyo, kocha wake hakuamini alichokiona kwa kiungo huyo na kuamua kuanza kumtania kwa kumwita jina la kiungo wa kifaransa, Ngolo Kante.

KAMBI POPOTE

“Shule niliyokuwa nikisoma ilikuwa ni ya bweni kwa hiyo niliondoka na nguo zangu zote nyumbani, nilianza kuzoea hapo maisha ya kukaa mbali na familia yangu sikuwa napata muda wa kutosha kukaa na wazazi.

“Sikupendelea kurudi nyumbani kipindi cha likizo na badala yake nilikuwa nikibeba nguo zangu na kwenda kwenye klabu yangu moja ya mtaani iitwayo Lujuma, nilikuwa nikiichezea, ilikuwa imejikamilisha kiujumla,” anasema.

Tangu hapo Ng’anzi anasema alizoea maisha ya kutangatanga kama mkimbizi huku akibeba nguo zake zote maana aliichezea timu yake katika mashindano mbalimbali ya kishule ambayo mengine iliwalazimu wasafiri nje ya mkoa wa Mwanza.

AKATISHA MASOMO

Kuitwa kwa Ng’anzi kwenye kikosi cha Serengeti Boys iliyoshiriki Afcon, Gabon kulimfanya kuyaweka kando kidogo masomo na kuanza kupigania ndoto zake za kutaka kuwa mcheza soka la kulipwa.

“Tulijiandaa kwa muda mrefu kama watu wanakumbuka hapo nilikuwa darasa la saba hapo ndipo nilipoamua kuachana na mambo ya shule kwa sababu tayari nilikuwa nimeona nafasi ya kutokea,” anasema kiungo huyo mkabaji.

MTEGO WA POULSEN

Wakati wa maandalizi ya Afcon , Ng’anzi anasema kocha wa kipindi hicho, Kim Poulsen ni kama alianza kwa kumtega ili atizame uwezo wake maana alikuwa akimtumia kama beki wa kati nafasi ambayo hakuwa akiifurahia.

“Nilikuwa nikicheza kwa kujituma lakini sikuwa na furaha na hiyo nafasi, ilitokea siku moja, aliyekuwa akicheza namba sita hakufanya vizuri ndipo mzungu alipoamua kuanza kunipanga.

“Dah!! Ni kama alifanya kosa vile maana nilionyesha uwezo mkubwa na tangu hapo sikuwahi kuchezeshwa wala kukaa nje kwenye kikosi cha Serengeti Boys, kuna kipindi nilikuwa nikipata maumivu lakini mzungu alikuwa akihimiza nichomwe sindano na kutumika,” anasema.

ALIVYOKWEA PIPA

Mwee!! Ng’anzi anasema mara yake ya kwanza kupanda ndege alikuwa na mawenge ya kuwaza itakuwaje kama ikianguka na ukingatia ndio kwanza safari yake ya soka imeanza.

“Kabla ya kuanza maandalizi ya Afcon ambayo kambi yake tuliweka nje ya nchi, nakumbuka nilisafari kwa mara ya kwanza kwa ndege kwenda India ambako kulikuwa na mashindano ya vijana ya Kimataifa yanayotambuliwa na FIFA.

“Siku moja kabla ya safari, tulikuwa tunakaa na wenzangu ile ndege ikipita tu juu ya anga tunaanza kupandwa na mizuka huku kila mmoja wetu akifurahia,” anasema Ng’anzi ambaye katika mashindano hayo walishika nafasi ya mshindi wa tatu.

MAMBO YALIVYOKUWA GABON

“Miongoni mwa matukio ambayo yameniumiza kwenye soka ni kushindwa kusonga mbele na kuishia hatua ya makundi nchini Gabon, wenzetu Niger walitushinda kikanuni.

“Uwezo wetu na wenzetu haukutofautina sana lakini naona wao walikuwa na wachezaji ambao miili yao ilikuwa mikubwa na imejengeka tofauti na sisi ambao tulikuwa na miili ya kawaida hilo halikututisha,” anasema.

GABON ILIMPA ULAJI

Wakati wa Afcon nchini Gabon, Ng’anzi anasema alipata Ulaji kutokana na kiwango chake kumvutia wakala wa Kikameroon, Alexandre Morfaw ambaye aliwahi kuzichezea klabu kadhaa kubwa barani Ulaya kama vile Leicester City na Nantes.

“Tatizo umri wangu ulikuwa chini ya miaka 17, ilikuwa ngumu kwangu kuchukuliwa, sikuelewa vizuri vipengele vyao lakini tuliendelea kuwasiliana kwa lengo la umri wangu ulisogea anisaidia kutimiza ndoto zangu,” anasema Ng’anzi.

KIDOGO ATUE YANGA

“Afcon ilivyomalizika Yanga ilikuwa timu ya kwanza ambayo ilionyesha nia ya kunihitaji, sikubabaika wala nini maana lengo langu lilikuwa ni kucheza Ligi Kuu kwa hiyo sikuangalia ukubwa wa klabu nilijisemewa timu itakayokuwa ya kwanza kunipa mkataba nitajiunga nayo.

“Walionyesha nia lakini walichelewa kunipa mkataba hivyo Singida United waliponiwahi sikuwa na chakupoteza zaidi ya kufanya maamuzi,” anasema.

SINGIDA WALIVYOMDAKA

“Aliyenitafuta alikuwa ni Sanga kupitia simu yake ya mkonini na kueleza kuwa wanatamani niwe mchezaji wa Singida, mara moja wakanifuata nilipo na kuongea ana kwa ana kisha nikasaini mkataba wa miaka mitatu.

“Nashukuru mungu, niliishi vizuri na nikajikuta nimekuwa rafiki wa Mudathir Yahya ambaye alikuwa ni kama injini ya Hans van der Pluijm, alinipa moyo kuwa ipo siku nitacheza na kweli ilitokeaga nafasi nikatumika kwenye Ligi kama beki wa kulia kwenye mchezo dhidi ya Majimaji ya Songea,” anasema.

WAKALA APAGAWA

Baada ya kumalizika kwa Afcon ya vijana, Morfaw aliendelea kumfuatilia Ng’anzi kwenye kikosi cha Ngorongoro Heroes hapo ndipo alipomvulia kofia kiungo huyo kwa kiwango alichokionyesha uwanja wa taifa kwenye mchezo dhidi ya DR Congo, Machi 31 mwaka jana.

“Nilicheza vizuri baada ya mechi alitoa ahadi ya kunipeleka Ulaya, nilifurahi sana na niliona mungu amefungia milango,” anasema.

MWIGULU AHUSIKA

“Uongozi wa Singida United, ulivyopata hizo taarifa za kupata wakala ambaye alikuwa tayari kunitafutia timu walifurahi na kusema watakuwa mstari wa mbele kuhakikisha kila kitu kinakwenda kama inavyotakiwa.

“Siku zilisogea na nikaambiwa nijiandae kuelekea Jamhuri ya Czech ambako ilipatikana timu, Morfaw alinisisitizia kuwa uwezo wangu nitakaoendelea kuonyesha utanifanya anipeleke timu kubwa zaidi,” anasema.

Ng’azi anasema miongoni mwa viongozi wa juu kabisa ambao wameonyesha sapoti ya kukamilika kwa dili lake ni  pamoja na mwanasiasa maarufu, Mwigulu Nchemba.

KUMBE NIZAR YUMO

Mbali na Mwigulu kuhusika kwenye dili la Ng’anzi kutua Jamhuri ya Czech pia nyota wa zamani wa Taifa Stars na Yanga, Nizar Khalfan kumbe naye amecheza nafasi kubwa ya kukamilika kwa uhamisho wa bwana mdogo huyo wa kujiunga na Vyskov ya daraja la pili nchini humo.

“Niligundua kuwa Nizar naye ni miongoni mwa watu muhimu kwangu, alikuwa akifanya mawasiliano na yule wakala na kila kitu kilivyokamilika aliniambia kuwa alicheza naye Vancouver Whitecaps FC   ya Canada ambayo imekuwa ikishiriki Ligi Kuu Marekani (MLS),” anasema.

ALIVYOTUA KIBABE ULAYA

Ng’anzi anasema baada ya kila kitu kikamilika alitua Jamhuri ya Czech na kukutana na mapokezi mazuri ambayo hakuyategemea huku akishangaa uzuri wa taifa hilo, anadai alipelekwa moja kwa moja hadi eneo ambalo alikuwa akikaa  kwa muda.

“Macho yanu yalikuwa yakishangaa miji mbalimbali ambayo tulikuwa tukikatisha, wenyeji wetu walikuwa wakitueleza majina ya kila mji ambao tuliupita hadi, Vyškov mjini,” anasema.

ALIANZIA KIKOSI B

“Nilianza kucheza kikosi B huko nilikuwa nikitizamwa na kocha msaidizi wa kikosi cha kwanza, nilicheza gamu kama tatu hivi, yule kocha aliukubali uwezo wangu ni wakaamua kunipeleka kikosi cha kwanza,” anasema.

KOCHA MKUBALI GHAFLA

Kiungo huyo wa Kitanzania, anasema mchezo wake wa kwanza kuwa benchi ulikuwa dhidi ya Rymarov, Oktoba 20 mwaka jana ambapo hadi unamalizika ugenini hakupata nafasi ya kucheza.

“Tulifungwa mabao 2-1, mchezo wa pili pia sikupata nafasi ya kucheza safari hiyo tulishinda kwa mabao 2-1, mchezo wa tatu nao sikupata nafasi, lakini nashukuru mungu ilikuwa Novemba, 10 tukiwa nyumbani nilicheza kwa dakika 17 tu.

“Dakika zile zilitosha kocha kunikubali kwa sababu nilichokuwa nakifanya ni kuhakikisha natoa sapoti kwa mabeki wa kati pia nilikuwa nikiachia mipira kwa haraka, penye ulazima wa kukaa nao nilifanya hivyo na kupiga mashuti mawili,” anasema

Ng’anzi anasema waliibuka na ushindi wa mabao 4-1 na anadai kuwa alijisikia furaha na baada ya mchezo huo, yakafuata mapumziko marefu ambayo yanamalizika mwishoni mwa mwezi huu  ambayo yalimfanya arejee nchini ili kusheherekea krisimasi na mwaka mpya.

WAMWITA NG’OLO KANTE

“Jamaa kazi yangu niliyoifanya ile siku walianza kuniita Ng’olo Kante, nadhani ni kwa sababu ya kuwa rangi yangu ni nyeusi na nimchezaji ambaye nacheza nafasi ambayo na yeye anacheza, natamani kufikia mafanikio yake,” anasema.

ASHANGAA GIZA MAPEMA

“Kilichonishangaza Jamhuri ya Czech ni giza kuingia jioni, sikuamini yani kule saa moja ni muda wa kulala kwa sababu mida ya saa 10 tu giza unakuta limeingia,” anasema.

KISA CHAKE SUPAMAKETI

Ingekuwa Supamaketi ya bongo, Ng’anzi anasema mbona ingekuwa freshi tu maana angerudisha baadhi ya vitu ili kuendana na kiwango cha fedha alichobeba kwa ajili ya kufanya manunuzi yake binafsi.

“Kilichotokea siwezi kusahau aiseeh maana nilienda mwenyewe sku hiyo kufanya manunuzi, wakati huo bado sijazijua vizuri hela zao kutumia, nilibeba kiasi ambacho nilihisi kinatosha.

“Siku huyo mtu ambaye amekuwa kama msaidizi wangu alikataa na kusema leo nimechoka nenda mwenye sasa nilifika na kuchukua nachotaka ile naenda kulipia hela kumbe haitoshi na kwa wenzetu huruhusiwi kurudisha vitu ambavyo tayari umeshachukua.

“Niliomba nikachukue kiasi kilichopelea nyumbani nilikimbia fasta na kurudi haraka na kisha nikamalizana nao tangu siku hiyo nimekuwa mzito kwenda mwenyewe kwenye manunuzi,” anasema Ng’anzi.

RATIBA YAKE KWA SIKU

“Kibaya ni kwamba kila mtu baada ya mazoezi yuko na mambo yake kwa hiyo sina kampani kama nyumbani ambapo nilikuwa Napata muda wa kutembea na marafiki zangu.

“Nachofanya baada ya mazoezi ni kurudi napokaa kupumzika na baadae naelekea gym kwa ajili ya kujiweka fiti, mazoezi tumekuwa tukifanya mara nyingi nyakati za asubuhi,” anasema.

KILUGHA CHAMCHANGANYA

Mbali na Kingereza ambacho kimekuwa kikitumika kwa mataifa mengi ya Ulaya, Ng’anzi anasema hakuna kitu kinachomuumiza kichwa kama kilugha ambacho kimekuwa kikitumika nchini humo mbacho ni Kislovak.

“Aisee!! Ni chenga tu, nikisikia ambao naongozana nao wanaanza kukizungumza nachofanya natoa simu yangu ya mkononi na kuweka phone masikioni kisha nasikiliza muziki mzuri wa nyumbani Tanzania,” anasema.

TRENI ZAMPAGAWISHA

“Wameendelea wenzetu treni zao utadhani ndege, Jamhuri ya Czech usafiri wao mkubwa ni treni kutoka mji mmoja kwenda mwingine, ni masaa machache unaweza kutumia kwenye safari ya umbali mrefu,” anasema.

VYAKULA MBONA FRESHI

Pamoja na kukumbuka vyakula vya nyumbani Tanzania ambavyo ndivyo vilivyomlea hadi anatimiza miaka 18, Ng’anzi anasema vyakula vya Jamhuri ya Czech havimsumbui kabisa.

“Zile safari za hapa na pale nikiwa na timu ya taifa ilinisaidia sana maana kuna aina ya vyakula ni vya kimataifa ambavyo ukienda kwenye mataifa yalitoendelea unakutana navyo,” anasema.

Ng’anzi alizitaja aina ya vyakula kwa lugha ya kigeni  ambavyo ni maarufu nchini humo, Side dishes, Soups, Meat dishes, Snacks, Sweets, Breads na pastries.

AWAKATAA WAREMBO KIAINA

Ng’anzi anasema amekuwa akikutana na mademu wakali wa kizungu lakini hana mapango nao kutokana na kutambua kuwa ili atimize ndoto zake anatakiwa ajitunze.

“Nikijiingiza huko nadhani utakuwa mwisho wa safari yangu ya soka, nafasi ninayocheza ya kiungo wa chini ni ngumu muda wote wa mchezo inanihitaji nisafe ili kuhakikisha tunakuwa imara,” anasema.

AITAKA MONACO

Ndoto za Ng’anzi ni kucheza soka la kulipwa Ufaransa na moja ya klabu ambayo anaihusudu ni AS Monaco ambayo anaichezea kiungo wa Kihispania, Cesc Fabrigas.

“Wakala wangu alicheza soka Ufaransa, aliniambia anaukaribu na timu nyingi za nchini humo, amekuwa akiniambia kuwa hakuna kinachoshindikana kikubwa ni kuweka juhudi,” ansema.

ANACHOVIMBIA WAKALA WAKE

Miongoni mwa vitu ambayo wakala wa  Ng’anzi, Morfwa anavyovimbia mbali na kuwasaidia vijana kibao wa Afrika Mgharibi   ni pamoja na kumsimamia kiungo   Moussa Sissoko wa Tottenham Hotspur  ya England.

AWASTUA VIJANA WENZAKE

Katika mahojiano yetu na Ng’anzi alimalizia kwa kuwataka vijana wenzake kutokata tama, waamini kuwa ipo siku ambayo jina anaijua mungu watatimiza ndoto zao za kupata nafasi ya kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.

“Adui namba moja wa mafanikio ni kukata tama, ikiwa wewe mwenye ndiye unayejikatisha tama basi tambua mchawi namba moja wa wewe kushinda kupiga hatua ni wewe mwenyewe.

“Muogope kama ukoma mtu anayekukatisha tama, kikubwa ni kuamini kuwa ipo siku, utatoboa,” anasema Ng’anzi kisha na kutudokezea kuwa yuko mbioni kuelekea Marekani.

Alicheka kiungo huyo wa zamani wa Singida United  na kusema yajayo yanafurahisha na kumalizia hiyo timu nimeshamalizana nayo ila kuna vitu vidogo vimesalia ila inashiriki Ligi Kuu Marekani ambayo ni maarufu kama MLS.