Kichuya akinukisha muda huu kwa Al Ahly

Muktasari:

Kichuya msimu uliopita alikuwa mmoja wa wachezaji tegemeo wa Simba na kuiongoza timu hiyo kutwaa ubingwa wa kwanza baada ya miaka 5.

Cairo, Misri. Winga wa kimataifa wa Tanzania, Shiza Kichuya ameanza katika kikosi cha kwanza ENPPI kinachoikabiri Al Ahly kwenye Uwanja wa Petro Sport, Cairo katika Ligi Kuu Misri.

Kichuya aliyejiunga kwa mkopo ENPPI mwishoni mwa wiki akitokea timu ya Pharco ya daraja la pili iliyomnunua kutokea Simba.

Winga huyo Mtanzania anacheza mechi hiyo akiwa na lengo la kulipiza kisasi baada ya timu yake ya zamani ya Simba mwishoni mwa wiki kupokea kipigo cha mabao 5-0 kutoka kwa Al Ahly katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hata hivyo hadi dakika 45 za kwanza zinamalizika ENPPI ya Kichuya ilikuwa nyuma kwa bao 1-0 kutoka Al Ahly.

Awali Kocha wa ENPPI, Ali Maher ambaye ni mchezaji wa zamani wa Ahly alisema timu yake inataka kushinda mchezo huo ili kujiweka vizuri katika ligi hiyo.

ENPPI kwa sasa ipo nafasi 14 ikiwa na pointi 21, endapo watapoteza mchezo huo watazidi kujiweka vibaya katik msimamo wa ligi hiyo.

Vikosi:

ENPPI: Amr Hossam, Ali Fawzi, Rami Sabri, Ahmed Saber, Amr El-Halawani, Mahmoud Toba, Mahmoud Ghali, Mohamed Ashraf, Ahmed Shoukri, Shiza Kichuya, Mahmoud Kaoud 

Ahly: Mohamed El-Shennawi - Mohamed Hani, Saad Samir, Ayman Ashraf, Ali Maaloul - Karim "Nedved" Walid, Amr El-Sulaya, Nasser Maher - Hussein El-Shahat,  Geraldo, Junior Ajayi.