Fainali ya kibabe Kariobangi, Bandari hapatoshi

Sunday January 27 2019

 

By OLIVER ALBERT

Dar es Salaam.Kocha mkuu wa Kariobangi Sharks, Willium Muluya amekiri mchezo wa leo Jumapili  wa fainali ya SportPesa dhidi ya Bandari utakuwa mgumu lakini watahakikisha wanashinda na kutwaa ubingwa.
Timu hizo zote zinazoshiriki Ligi Kuu Kenya zitacheza fainali hiyo Uwanja wa Taifa Dar es Salaam itakayoanza saa 10:00 jioni ikitanguliwa na mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu kati ya Simba na Mbao zote za Tanzania.
Kariobangi na Bandari zimekutana mara mbili mwaka jana kwenye Ligi yao na mchezo wa kwanza Kariobangi iliifunga Bandari bao 1-0 na mchezo wa pili ilichapwa na Bandari mabao 3-0.
Pia jambo la kuvutia kwa timu hizo ni kwamba zote hazijapoteza mchezo kwenye Ligi ingawa Bandari iko nafasi ya pili  ikiwa na pointi 18 baada ya kucheza michezo nane, imeshinda mitano na kutoa sare mitatu wakati Kariobangi Sharks iko nafasi ya tano ikiwa na pointi 14 baada ya kucheza michezo nane, imeshinda mitatu na kutoa sare mitano.   
Muluya alisema kitu kinachovutia ni kwamba timu zinazocheza fainali zinafahamiana hivyo utakuwa mchezo mzuri na wenye ushindani mkubwa.
"Itakuwa mechi nzuri na yenye kuvutia sana kwani tunajuana.Tumecheza Ligi ya Kenya na kila mmoja alimfunga mwenzake hivyo kila timu ina kiwango.
"Malengo yetu ni kuchukua ubingwa na kupata nafasi ya kucheza na Everton ya England.Hatutakubali kupoteza hii nafasi hivyo wachezaji wangu wanajua umuhimu wa hii mechi na naamini hawataniangusha"alisema Muluya.

Advertisement