Yanga yaifanya kitu mbaya Mwadui

Muktasari:

Licha ya Yanga kuwa mbele kwa magoli mawili, Mwadui walionekana kuumiliki mpira na kufanya mashambulizi ya mara kwa mara langoni mwa Yanga.

Dar es Salaam. Mabao ya Ibrahim Ajib na Amis Tambwe yamewatanguliza kifua mbele Yanga katika dakika 45 za kipindi cha kwanza.

Katika mchezo huo timu zote zilianza kwa kasi huku wote wakionekana kutaka bao la mapema katika mchezo huo.

Hata hivyo, Yanga iliweza kupata magoli mawili na kwenda mapumziko wakiwa wamejihakikishia ushindi nusu dhidi ya Mwadui.

Dakika 3, Salim Aiye alipiga shuti ndani ya boksi baada ya kuonganishiwa pasi na Ditram Nchimbi, hata hivyo shuti hilo lilipanguliwa na Klaus Kindoki na kuwa kona isiyokuwa na faida.

Ndani ya dakika 11, Yanga hawakuliona lango la Mwadui mpaka dakika hiyo hiyo Ibrahim Ajib kufunga kwa faulo baada ya Mrisho Ngassa kudondosha nje ya kumi na nane.

Hata hivyo Mwadui waliendeleza mashambulizi na dakika 14 Ditram nchimbi alipiga shuti lakini lilitoka pembezoni kidogo kwenye goli lao.

Safu ya ulinzi kwa upande wa Yanga ilikuwa ikikatika mara kwa mara kiasi ambacho waliwaruhusu washambuliaji wa Mwadui, Ditram Nchimbi na Salim Aiyee kuingia ndani ya 18 mara kwa mara.

Yanga ilipata penalti dakika 17 baada ya beki wa Mwadui, Frank John kufanya madhambi kwa Tambwe, lakini hata hivyo penalti hiyo iliyopigwa na Ajib iliishia mikononi mwa Arnold Massawe.

Kipa wa Yanga, Klaus Kindoki katika mchezo huu alikuwa na makosa ya mara kwa mara kiasi ambacho kilimlazimu kocha Mwinyi Zahera kufanya nae kikao kifupi wakati mchezo huo ukiendelea.

Mwadui walizidi kuutawala mchezo kwa kufanya mashambulizi ya haraka haraka kiasi ambacho kilionekana kuwapa presha safu ya ulinzi Yanga, lakini hata hivyo hawakuweza kuweka mpira wowote wavuni.

Mshambuliaji wa Yanga, Ajib alitolewa nje na muamuzi Fikiri Yusuph baada ya kuvaa tait rangi tofauti lakini alipobadilisha alirejea uwanjani.

Yanga licha ya kuongoza kwa goli moja walikuwa wanacheza kwa kujilinda zaidi huku wakishambulia kwa kuvizia wakati Mwadui walikuwa wakifunguka na kushambulia kwa mfululizo.

Yanga ilipata bao la pili baada ya Tambwe kuonganisha kwa kichwa krosi iliyopigwa na  Ajib na kuwanyanyua mashabiki kwa bao hilo.

Baada ya bao hilo kuingia wachezaji wa Mwadui walikaa kikao cha takribani sekunde 20 kujadiliana kilichotokea uwanjani hapo.

Yanga nao waliamua kufunguka ndani ya dakika tano za mwisho na dakika 45 walifanya shambulizi la kushtukiza baada ya Mrisho Ngassa kupenyezewa pasi na kuwazidi spidi mabeki wa Mwadui na kufanikiwa kuingia ndani ya 18 hata hivyo alipiga pasi ya mwisho kwa Amis Tambwe lakini mchezaji huyo alipiga shuti lililomgonga kipa na kuondolewa golini na mabeki wa Mwadui.