Msolla: Kindoki hafai, Kakolanya kaharibu

Muktasari:

Beno Kakolanya alijingua kwenye kikosi chake cha Yanga akishinikiza kulipwa pesa zake za usajili Sh 15 milioni na mishahara yake ya miezi minne na kukosa mechi nne ambazo Yanga walicheza na kushinda zote na sasa amelipwa mishahara ya miezi miwili na Sh 2 milioni za usajili lakini kocha wake Mwinyi Zahera ameweka ngumu kumpokea mchezaji huyo.

Dar es Salaam.WAKATI sakata ya kipa Beno Kakolanya dhidi ya Yanga likiwa halijapoa, ikielezwa kocha wake, Mwinyi Zahera amegoma kumpokea, kocha maarufu nchini Mshindo Msolla naye ameibuka na kupigilia msumari.

Wakati akipigilia msumari kwa kakolanya pia amemuweka wazi kuwa Kocha Zahera amechemka kumsajili kipa wake, Klaus Nkinzi Kindoki kwani naye hafai kuwepo ndani ya Yanga.

Dk Msolla alisema maamuzi anayoyafanya Zahera ni sahihi na hapaswi kupingwa wala kuingiliwa kwa kile alichokieleza ameonyesha utovu wa nidhamu ndani ya Yanga.

Msolla alisema Kakolanya alipaswa kuilipa fadhila Yanga kwani kipindi ambacho amejiunga Yanga amekuwa mchezaji mwenye kuandamwa na majeraha, lakini uongozi ulikuwa ukijali hilo na kumlipa mishahara yake kama kawaida hata akiwa nje ya uwanja kwa kipindi kirefu.

"Inawezekana amekosa washauri wazuri wa kumwelekeza jinsi ya kudai haki yake ndani ya klabu, kiufundi naungana na Zahera kwa asilimia 100 kwani mchezaji kama huyo anaonyesha utovu wa nidhamu ambapo kiufundi unaiathiri timu, hata mimi nisingekubaliana naye.

"Nilikuwa namwangalia Beno (Kakolanya) kama miongoni mwa wachezaji bora na wenye uwezo mkubwa sana kisoka hapa nchini maana kuna baadhi ya vitu amemzidi hata Aishi Manula, ila mwenzake hana tabia kama alizozionyesha kutokuwa na fadhira kwa timu yake.

"Binafsi huwa nasimamia sana nidhamu nilipokuwa kocha, kiukweli asingepata tena nafasi ya kuichezea timu yangu, anapaswa kuachwa na kwenda kutafuta maisha sehemu nyingine ambayo hawatakwama kumlipa," alisisitiza Dk Msolla.

Mtaalamu huyo alisema kitendo hicho kitamwathiri mchezaji kwani hata timu ya Taifa atakosa nafasi maana hakuna kocha anayeita mchezaji asiyekuwa na nidhamu na hachezi sehemu yoyote.

"Sasa hivi ni ngumu sana kumpa nafasi Taifa Stars na hakuna kocha anayeweza kumuita mchezaji asiyecheza, alipaswa kukumbuka wakati Yanga ina pesa na analipwa hata akiwa nje akiuguza majeraha yake, hawakumtupa sasa hivi anashindwa kulipa, alipaswa kumweleza matatizo yake mwalimu wake, wengi tumelea wachezaji wenye matatizo makubwa ya kifamilia pengine kuliko hata yake, ila tuliwajenga kutokana na hali halisi ya klabu zetu.

"Kingine ambacho kinapaswa kuangaliwa ni mpasuko unaoweza kujitokeza ndani ya timu baada ya Beno kulipwa pesa na mdau wa Yanga wakati wengine nao wanadai, utaratibu uliotumika sio mzuri kwa afya ya michezo, wanampoteza bila yeye kujua kuwa anatumika na Wanasiasa," alieleza

ZAHERA ACHEMKA

Wakati akisema Kakolanya hapaswi kuendelea kuwepo kikosi, lakini Dk Msolla amemweleza Zahera kuwa katika usajili aliochemka basi ni kumsajili kipa Kindoki.

"Yaani kama hawajafanya usajili nafasi ya kipa kipindi cha usajili wa dirisha dogo, basi kutakuwa na shida kwa kumtegemea Ramadhan Kabwili pekee kwani usajili wa Kindoki ndiyo usajili mbovu alioufanya Zahera, naye hafai kuwepo Yanga.

"Kabwili ni mzuri ila naye ni binadamu anaweza kuumwa ama kupata tatizo lolote ambapo itakuwa shida kwa Yanga na labda hicho ndicho kinachompa kiburi Beno kwamba hata akifanya mambo kinyume na taratibu za kazi basi atarejeshwa tu," alisema Dk Msolla.

Yanga ilikuwa katika mchakato wa kumsajili kipa wa timu ya Bandari FC ya Mombasa, Faruk Shikalo lakini usajili huo ulishindikana kutokana na masharti waliyopewa kwani alikuwa na mkataba na klabu yake.

Kakolanya atimuliwa mazoezini

Jana Jumamosi, Kakolanya alikwenda kwenye mazoezi ya Yanga ili kuonana na kocha wake lakini bila kutarajia alijikuta akitimuliwa.

Meneja wake, Haroub Seleman alisema; "Asubuhi aliniambia anaenda mazoezini, ila baadaye nilipompigia alinieleza kufukuzwa na kocha wake na kuambiwa hamuhitaji aende sehemu nyingine anayoweza kucheza.

"Nimezungumza na viongozi wa Yanga ambapo tumegundua pande zote mbili tumekosea, hivyo wameniahidi kulifanyia kazi ikiwemo kuzungumza na kocha wao, ila maamuzi yote yapo mikononi mwao, watakachoamua sisi tupo tayari.

"Wakati anakwenda kuonana na hao wadau waliompa pesa alinieleza na nilimruhusu kwani ni kawaida kwa hizi timu wachezaji kuchangiwa na wadau, kama kuna mengine nyuma ya pazia sikujua, kilichonipa imani kumruhusu ni baada ya kunitajia majina ya wachezaji wa zamani wa Yanga, hivyo sikuwa na hofu," alisema Haroub

Mratibu wa Yanga, Hafidh Salehe alisema mchezaji huyo labda ataanza mazoezi keshokutwa Jumanne kwani mambo yake na viongozi yapo vizuri bado upande wa kocha pekee.