Waziri Shonza aimiza michezo Chikota Cup

Thursday December 6 2018

 

By Haika Kimaro

Mtwara. Vijana wametakiwa kushiriki katika michezo mbalimbali ili kujipatia ajira na kujiepusha na magonjwa yanayoambukiza na yasiyoambukiza.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Juliana Shonza wakati akizindua mashindano ya Chikota Jimbo cup yaliyoandaliwa na Mbunge wa Nanyamba, Abdallah Chikota katika halmashauri ya mji Nanyamba.

Amesema kuibuliwa kwa vipaji kutasaidia kuchochea maendeleo na kuwataka viongozi wa michezo kutekeleza wajibu wao badala ya kuonekana tu wakati wa matukio.

“Michezo ni ajira ukiwa na kipaji popote utaonekana, sasa sitaki viongozi wa sherehe, maafisa michezo fanyeni kazi zenu piteni shuleni kuibua vipaji… kama yupo asiyefanya kazi ajitathimini,” amesema Shonza

Aidha wadau wa michezo wametakiwa kuanzisha mashindano mbalimbali ili kuibua na kukuza vipaji.

Mbunge wa jimbo la Nanyamba, Abdallah Chikota amesema kuanzishwa kwa mashindano hayo kutaibua vipaji, pia kutoa ajira na kuimarisha mashikamano ndani ya jamii.

“Jamii inapokuwa inajihusisha na michezo ushirikiano katika masuala mbalimbali unaimarika inakuwa ni rahisi pia katika uzalishaji kwa sababu mtu anapofanya mazoezi anaweka mwili fiti hata magonjwa yasiyoambukiza inakuwa sio rahisi kumnyemelea,”amesema Chikota

Aidha ameahidi kuwaendeleza katika shule za vipaji vijana watakaoshinda ili waweze kuonyesha vipaji vyao ndani na nje ya nchi.

Mmoja wa wachezaji wa timu ya Kiromba, Zerafi Suleiman amesema kuanzishwa kwa michuano hiyo kutasaidia kuwatangaza na kujipatia ajira.

“Mashindano haya ni mwanzo wa kujitangaza na kuonyesha vipaji’ niziombe na klabu nyingine kubwa nchini wasisite kucheza na sisi michezo ya kirafiki wanapokuja katika mkoa wetu, lengo ni kuimarisha vipaji,” amesema Suleiman

Advertisement