Bunge Queens yagawa dozi michezo ya Mabunge

Tuesday December 4 2018

 

By Imani Makongoro

Dar es Salaam.Timu ya Netiboli ya Bunge la Jamhuri ya Muungano (Bunge Queens) imefanya 'mauaji' katika mashindano ya Mabunge Afrika Mashariki yanayoendelea nchini Burundi.

Bunge Queens imetembeza kipigo cha magoli 87-8 kwa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) huku kaka zao The Dons wakiduwazwa kwa kipigo katika mpira wa wavu.

Katika mchezo huo uliopigwa kwenye viwanja vya Chuo cha Taifa cha Ualimu cha Burundi umerejesha nguvu mpya kwa Bunge Queens ambayo ilianza kwa kipigo dhidi ya Uganda.

Akizungumza baada ya mchezo huo, mchezaji wa Bunge Queens, Anna Gidarya ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Netiboli Tanzania Chaneta, alisema walijipanga kushinda baada ya kupoteza mchezo wa awali ndiyo sababu waliwatembezea kipigo hevi wenzao wa EALA.

Wakati Bunge Queens wakitamba, kaka zao waliambulia kipigo cha seti 3-0 kwenye mpira wa wavu kutoka kwa Kenya.

Timu ya Mpira wa Wavu (wanaume ) imejikuta ikipokea kipigo cha seti 3-0 kutoka kwa Kenya.

Msemaji wa Bunge Sports Club, Cosato Chumi (Gaza) ambaye ni mbunge wa Mafinga Mjini alisema wamejipanga kufanya vizuri katika mashindano hayo katika michezo mbalimbali ikiwamo soka na riadha.

Advertisement