Kimbunga Aubameyang chaikumba Spurs, Arsenal yaua

Muktasari:

Ushindi huo unaifanya Arsenal kupanda hadi nafasi ya nne huku Spurs ikiporomoka kutoka katika nne bora

London, England. Arsenal imethibisha ubora wa safu yake ya ushambuliaji baada ya kuichakaza Tottenham Spurs kwa mabao 4-2 kwenye Uwanja wa Emirates.

Kikosi cha kocha Unai Emery kimeendeleza rekodi yake ya kutofungwa katika mechi 19, imeishusha Spurs katika nne, baada ya kuonyesha soka ya kiwango cha juu chini ya Mhispania huyo anayeoneka kuvivaa vizuri viatu vya Arsene Wenger.

Arsenal ilikuwa ya kwanza kupata bao lililofungwa na Pierre-Emerick Aubameyang kwa mkwaju wa penalty baada ya beki Jan Vertonghen kushika mpira.

Lakini Spurs ikirudi mchezoni na kufanikiwa kupata mabao mawili ya haraka kupitia Eric Dier aliyefunga kwa kichwa akiunganisha mpira wa adhabu wa Christian Eriksen, wakati akishangilia bao hilo kulisababisha mvutano baina ya wachezaji wa timu hizo mbili.

Spurs ilipata bao la pili lililofungwa kwa mkwaju wa penalty na Harry Kane iliyotokea baada ya Rob Holding kumchezea vibaya Son Heung-min.

Kocha Emery aliwaingiza Alexandre Lacazette na Aaron Ramsey mwanzoni mwa kipindi cha pili mabadiliko yaliyokuwa na faida kwa wenyeji.

Ramsey alitegeneza bao la pili la Aubameyang, kabla ya Mfaransa Lacazette kupachika bao la tatu kwa shuti lake kumgongo beki na kupoteza kipa Hugo Lloris na kujaa wavunia kuifanya Arsenal kuongoza 3-2 zikiwa zimebaki dakika 16.

Kiungo Lucas Torreira likimbia na mpira kutoka pembeni na kupiga shuti lililojaa wavuni na kuipa Arsenal ushindi mnono wa mabao 4-2, katika dakika za mwisho Vertonghen wa Spurs alitolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kumchezea vibaya Lacazette.