EMERY, POCHETTINO USHKAJI WEKA KULE!

Muktasari:

Makocha hao waliwahi kufanya kazi huko Hispania, ambapo Emery alimpendekeza Pochettino awe mrithi wake kwenye kikodi cha Valencia mwaka 2012

LONDON, ENGLAND.Mauricio Pochettino amesema anaamini urafiki wake na Unai Emery hauwezi kufa kisa kitakachotokea huko Emirates wakati timu zao zitakapochuana kwenye mchezo wa Ligi Kuu England leo Jumapili.

Pochettino na kikosi chake cha Tottenham Hotspur kitakwenda Emirates kuwavaa mahasimu wao Arsenal wanaoonolewa na Emery mechi hiyo itawakutanisha maswahiba wawili walioshibana.

Makocha hao waliwahi kufanya kazi huko Hispania, ambapo Emery alimpendekeza Pochettino awe mrithi wake kwenye kikodi cha Valencia mwaka 2012.

Lakini, sasa wamekuwa wapinzani kwenye Ligi Kuu England na mbaya zaidi wanazinoa timu mahasimu wa huko London Kaskazini.

Akiulizwa kama urafiki wao utatibuka, Pochettino alisema: "Mimi nawaza tofauti. Sawa tupo kwenye klabu tofauti na hii ni dabi, hivyo ni lazima tucheze.

"Jambo moja ni kumalizana tu. Lazima tumalizane na tutajaribu kushinda kwa njia yoyote ile na baada ya mechi nadhani tutabaki kuwa marafiki."

Hii ni mechi ya kwanza kwa maswahiba hao kukutana kwenye Ligi Kuu England na jambo hilo linasubiriwa kwa hamu kuona kitu kitakachotokea.

Hakuna ubishi wawili hao ni marafiki kiasi cha kumfanya hata Emery kumuuzia Pochettino wachezaji wawili matata, Lucas Moura na Serge Aurier wakati alipokuwa kwenye kikosi cha Paris Saint-Germain.

Emery aliamua kumpa silaha hizo rafiki yake awatese kwenye Ligi Kuu England kabla ya yeye mwenyewe kukubali kazi ya kwenda kuwa mrithi wa Arsene Wenger huko Emirates.