Mtibwa Sugar wala hawana noma yaani!

Muktasari:

Kikosi cha Mtibwa Sugar mabingwa wa Ligi Kuu Bara mara mbili mfululizo kwa mwaka 1999 na 2000, inashiriki mashindano ya CAF baada ya zaidi ya miaka 10, kupita.

Dar es Salaam. Mtibwa Sugar ipo tayari kuivaa Northern Dynamo ya Shelisheli na watawapa raha Watanzania, na kusisitiza hawatafanya usajili wa dirisha dogo labda kama itatokea wenye fedha Simba na Yanga watawaharibia.

Mtibwa Sugar inajiandaa na mchezo wao wa Kombe la Shirikisho Afrika na timu hiyo ya Shelisheli inayotarajiwa kucheza kati ya Novemba 27 na 28 na watakuwa nyumbani na wa marudiono ni kati ya Desemba 4 na 5, ugenini.

Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Zubery Katwila amesema, kila kitu kinakwenda sawa: "Wakati tunafanya maandalizi na kucheza mechi za Ligi Kuu tulikuwa tunajiandaa pia na mashindano haya ya CAF."

Awali, Mtibwa Sugar walikuwa na mpango wa kucheza mechi tatu za kirafiki lakini mpaka sasa bado, Katwila amesema: "Tulikuwa na mpango huo lakini tukakosa mechi kama tutapata ndani ya kipindi hiki tutacheza."

Akizungumzia dirisha dogo la usaji lililoanza Novemba 15, na litafungwa Desemba 15, Katwila amesema: "Kikosi chetu ni hicho, lakini huwezi kujua maana wapo wanaotuharibia mipango yetu mara kwa mara hasa hizo timu zenu zenye pesa. Ikitokea wakatuchukulia wachezaji wetu na sisi tutasajili."

Kocha huyo ambaye pia anainoa timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 23, hakuzitaja kwa majina, lakini inajulikana kuwa miongoni mwa klabu hizo ni Simba, Yanga na Azam FC.