Wazee wa benchi Simba, Yanga wamkera Amri Said

Muktasari:

Kocha wa Mbao FC, Amri Said ameshangazwa na wachezaji ambao wameganda Simba na Yanga licha ya kukaa benchi, kitendo alichokiita ni kutojielewa kwa sababu umri wao unaenda.

Dar es Salaam. Kocha Mkuu wa Mbao FC, Amri Said amesema kuna wachezaji wa ajabu nchini wapo tayari kukaa benchi katika timu za Simba na Yanga na kula mshahara wasioutolea jasho wakati kuna timu zinazohitaji huduma yao.

Amri aliyewahi kuichezea na kuifundisha Simba miaka ya nyuma amesema, amekumbana na jambo hilo pindi alipokuwa anahitaji huduma ya baadhi ya wachezaji hao, lakini wanakataa na madai yao hawawezi kuishi mikoani.

"Sasa unakuwa unajiuliza hawa wachezaji wanataka kufika wapi? Furaha yao ni kuvaa jezi tu na maisha mazuri ya mjini maana kuna mwisho wa hayo na ndiyo maana kina Amri leo hii ni makocha na si wachezaji," alisema Amri.

"Kikubwa wachezaji wajielewe na kujua muda ni mali, ni kweli wanapata sifa kuonekana ni wachezaji wakubwa na ustaa ambao unatoka kwa mashabiki, lakini mwisho wa siku baada ya hapo maisha yao yanakuwa vipi kama soka ni njia ya kupatia uchumi waheshimu, ila wakitaka sifa basi waendelee," anasema kocha huyo.